Home » » POLISI MOSHI VINARA KUSAFIRISHA MAHARAMIA

POLISI MOSHI VINARA KUSAFIRISHA MAHARAMIA


na Charles Ndagulla, Moshi
MAOFISA Uhamiaji katika kituo cha Holili wilayani Rombo na maofisa wa polisi katika vituo vya polisi Holili na Himo, wametajwa kuwa vinara wa biashara ya kusafirisha wahamiaji haramu.
Uchunguzi uliofanywa na Tanzania Daima Jumatano, umebaini kuwa maofisa hao wa serikali ndio wanaohusika na utoaji wa ‘njia’ ambazo huwawezesha wasafirishaji kupita bila kukamatwa.
Kupitia utoaji huo wa njia, kila mwenye kusafrisha binadamu hao ambao wengi wao wanatoka katika nchi za Somalia na Eithiopia, maofisa hao hulipwa pesa taslimu kati ya sh 300,000 na sh 500, 000 kwa kila gari.
Pesa hizo zinajulikana kwa jina la kusafisha ‘njia’ na baada ya wahusika kutoa fedha hizo, hupewa maelekezo ya njia za kupita pamoja na muda, na wakati huo magari ya doria huondolewa maeneo husika.
Mbali ya hilo, baadhi ya polisi katika vituo vya Tarakea, Holili na Himo wamekuwa wakitumia magari yao madogo aina ya Toyota Noah kusafirisha wahamiaji haramu na huwa hayakamatwi kutokana na askari hao kufahamiana na askari wa doria.
Katika tukio la Julai 27 mwaka huu, askari wa kituo cha polisi Himo, wakiwa na maofisa uhamiaji wa kituo cha Holili, waliliachia gari aina ya Toyota Noah lenye namba za usajili T 324 BRG, mali ya Mary Kundy wa mjini Moshi likiwa na wahamiaji haramu 14.
Baada ya kulizingira gari hilo saa 6 usiku eneo la njia panda ya Himo, askari hao waliwaondoa wahamiaji hao haramu kutoka kwenye Noah na kuwaingiza kwenye gari la mkuu wa kituo cha polisi Himo na kuwasafirisha hadi Moshi mjini.
Hata hivyo, Kamanda wa Polisi Mkoa wa Kilimanjaro, Robert Boaz, amekuwa akiwatetea askari wake akidai kuwa, gari hilo lilitumika kufanikisha ukamataji wa wahamiaji hao.
Vijiji ambavyo vimegeuzwa mapito ya wahamiaji haramu katika Wilaya ya Moshi Vijijini, ni Lotima, Kilototoni, Ghona, Makuyuni na Chekereni ambako baadhi ya nyumba hutumika kuwahifadhi wahamiaji hao na kuwahudumia kwa chakula na maji.
Kwa upande wake Mkuu wa Mkoa wa Kilimanjaro, Leonidas Gama amewaonya watumishi wa serikali kuacha kujihusisha na usafirishaji wa wahamiaji haramu na kusisitiza hatosita kuwachukulia hatua za kinidhamu.
Chanzo: Tanzania Daima

0 comments:

 
Supported by Tone Multimedia Company Limited
Copyright © 2012. Kilimanjaro Yetu - All Rights Reserved
Designed by Fredy Tony Njeje
Proudly powered by Blogs za Mikoa