Home » » RAIA WA LITHUANIA MBARONI KWA DAWA ZA KULEVYA

RAIA WA LITHUANIA MBARONI KWA DAWA ZA KULEVYA



Na Upendo Mosha, Moshi
RAIA mmoja wa kigeni wa nchini Lithuania, anashikiliwa na Jeshi la Polisi mkoani Kilimanjaro baada ya kupatikana na shehena ya dawa za kulevya aina ya cocaine zenye uzito wa kilo 4.4.

Kamanda wa Polisi, Mkoa wa Kilimanjaro, Robert Boaz, alisema jana, kuwa mtuhumiwa Kristina Biskasevskaja (20), alikamatwa Agosti 28 mwaka huu, saa 9 mchana katika Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Kilimanjaro (KIA).

Alisema mtuhumiwa alikamatwa akiwa na sanduku lenye dawa hizo.

Alisema Biskasevskaja alikuwa akisafirisha dawa hizo kwenda nchini Ubeligiji kwa ndege ya Shirika la Ethiopia yenye namba 0814 na kwamba alikuwa akitaka kupitia jijini Addis-Ababa, Ethiopia.

Alisema, kabla mtuhumiwa huyo hajakamatwa, wakati akiingia uwanjani hapo sanduku lake lilitiliwa shaka na alipopekuliwa alikutwa na dawa hizo.

“Uchunguzi wa kina na wa kitaalamu juu ya tukio hili bado unaendelea ili kubaini thamani halisi ya dawa hizo na mtuhumiwa bado anashikiliwa akisubili kufikishwa mahakamani muda wowote baada ya taratibu zote kukamilika,” alisema Kamanda Boaz.

Aidha, Kamanda Boaz alisema, dawa hizo ambazo zinadhaniwa kuwa ni aina ya cocaine zimekuwa ni tatizo sugu katika nchi zinazoendelea na kwamba Jeshi la Polisi limejipanga vizuri ili kudhibiti biashara hiyo.
Chanzo: Mtanzania

0 comments:

 
Supported by Tone Multimedia Company Limited
Copyright © 2012. Kilimanjaro Yetu - All Rights Reserved
Designed by Fredy Tony Njeje
Proudly powered by Blogs za Mikoa