Mwansihi wetu, Rombo-Kilimanjaro Yetu
Kundi kubwa la tembo wanaokadiriwa kufika 200, limevamia kijiji cha Chala katika Wilaya ya Rombo Mkoani Kilimanjaro na kufanya uharibifu mkubwa wa mazao na makazi huku wakisababisha kifo cha mtu mmoja katika kijiji cha Mahida Nguduni.
Afisa Wanyamapori katika wilaya ya Rombo Edward Kileo amesema tembo hao wametokea katika Hifadhi ya Taifa ya Tsavo iliyoko kusini mashariki mwa nchi jirani ya Kenya na kuwa wamekuwa wakihama kutoka eneo moja hadi jingine kutafuta malisho na maji.
Amevitaja vijiji vilivyoathiriwa na tembo hao kuwa ni Mahida Nguduni, Ngoyoni, Ngareni, Mamsera na Holili huku mazao yaliyoathiriwa ni pamoja na ndizi ambacho ni moja ya chakula kikuu katika wilaya ya Rombo.
Kutokana na hali hiyo Mkurugenzi Mtendaji wa halmashauri ya wilaya ya Rombo Judethadeus Mboya amewataka wananchi katika wilaya ya Rombo kuuanza ufugaji nyuki ambao wanadaiwa kuwa adui wa tembo.
Hii ni mara ya kwanza katika kipindi cha zaidi ya miaka 20 kwa kundi kubwa la tembo kuvamia wakazi wa eneo hilo na wataalamu wa idara ya wanyamapori wamekuwa wakiwaasa wananchi kuepuka kuweka makazi ya kudumu katika maeneo jirani na ushorobo wa kitendeni ambako inasadikiwa ni njia ya asili ya tembo hao.
Kulingana na duru za kitafiti tembo hao wamekuwa wakiishi maisha ya kuhamahama kutoka hifadhi za taifa za Tsavo na Amboseli zilizoko kusini mashariki mwa nchi jirani ya Kenya na kuja katika hifadhi ya taifa ya mlima Kilimanjaro kwa upande wa Tanzania ikiwa ni sehemu ya mapito yao yanayokidhi mfumo wao wa kiikolojia.
Blogzamikoa
0 comments:
Post a Comment