Home » » WAKONGWE WAJITOKEZA KUWANIA UONGOZI CCM

WAKONGWE WAJITOKEZA KUWANIA UONGOZI CCM


na Dixon Busagaga, Moshi
MBIO za uchaguzi ndani ya Chama Cha Mapinduzi (CCM), zimezidi kushika kasi baada ya makada waliokuwa wamepotea katika medani ya siasa kwa muda mrefu, kujitokeza tena kuwania nafasi ya uenyekiti wa chama hicho Mkoa wa Kilimanjaro.
Miongoni mwa makada waliojitokeza ni aliyekuwa Mwenyekiti wa CCM Wilaya ya Moshi Mjini, Faraji Swain na Mchungaji wa Kanisa la Kiinjili la Kilutheri Tanzania (KKKT), Dayosisi ya Pare, Elisa Mrutu na kufanya idadi ya wanachama waliochukua fomu kufikia sita. Mchungaji Mrutu kwa sasa ni mjumbe wa Kamati ya Siasa Wilaya ya Same pamoja na Mjumbe wa Halmashauri Kuu ya CCM wilayani humo.
Wanachama wengine waliojitokeza kuwania nafasi hizo ni Peter David aliyewahi kushika nafasi ya uenyekiti wa CCM katika mkoa huo miaka ya nyuma, Mildred Kisamo na Daudi Nguzo.
Akikabidhi fomu kwa wanachama hao kwa niaba ya Katibu wa CCM Mkoa, Katibu Msaidizi wa mkoa, Kurwa Mmemo, aliwataka wote wanaoomba nafasi hizo kuzingatia kanuni na maadili ya chama, hasa katika kipindi hiki cha mchakato wa chaguzi za ndani.
Baadhi ya wanachama waliochukua fomu walielezea nia yao ya kuleta mabadiliko ya kisiasa yatakayokivusha chama hicho kutoka hapa kilipo na kuweza kuendeleza ushindi kwenye chaguzi mbalimbali.
Chanzo: Tanzania Daima

0 comments:

 
Supported by Tone Multimedia Company Limited
Copyright © 2012. Kilimanjaro Yetu - All Rights Reserved
Designed by Fredy Tony Njeje
Proudly powered by Blogs za Mikoa