Home » » AKAMATWA NA KETE 24 ZA DAWA ZA KULEVYA

AKAMATWA NA KETE 24 ZA DAWA ZA KULEVYA



Na Fadhili Athumani, Moshi
MFANYABIASHARA mmoja, Mkazi wa Pasua, Wilaya ya Moshi, mkoani Kilimanjaro, anashikiliwa na Jeshi la Polisi kwa tuhuma za kukutwa na kete 24 za dawa za kulevya.

Kwa mujibu wa taarifa ya polisi mkoani hapa mfanyabiashara huyo, Evance Cornel (29) alikamatwa jana usiku katika maeneo ya Shanty Town, Manispaa ya Moshi.

Sambamba na hilo katika Kata ya Jipe, wilayani Mwanga, mkoani hapa polisi inawashikilia watu 24, raia wa Ethiopia wanaodhaniwa kuwa ni wahamiaji haramu.

Wahamiaji hao wenye umri kati ya miaka 17-32 walikamatwa katika doria lililoendeshwa na mkuu wa upelelezi wa wilaya ya Mwanga, ambapo watuhumiwa wote wanashikiliwa katika kituo cha polisi cha Wilaya ya Mwanga.

Akithibitisha kutokea kwa matukio hayo, Kamanda wa Polisi mkoani Kilimanjaro, Robert Boaz, alisema watuhumiwa wote wanashikiliwa na Jeshi la Polisi na uchunguzi unaendelea.

Kamanda Boaz alisema dawa hizo zilizokamatwa zitafikishwa kwa mkemia mkuu wa Serikali kutambua ni aina gani ya dawa za kulevya.

“Tayari taratibu za kuhakikisha dawa hizo kupelekwa kwa mkemia mkuu wa Serikali yameshakamilika na wakati hayo yakiendelea pia tuko katika operesheni ya kuhakikisha Ramadhani na Familia yake wanakamatwa,” alisema.

Kamanda Boaz aliwataka wananchi kuwa makini na watu wanaoingia na kutoka katika maeneo wanayoishi, huku akisisitiza umuhimu wa Polisi kushirikiana bega kwa bega na wananchi katika harakati za kutokomeza uhalifu mkoani hapa.
Chanzo: Mtanzania

0 comments:

 
Supported by Tone Multimedia Company Limited
Copyright © 2012. Kilimanjaro Yetu - All Rights Reserved
Designed by Fredy Tony Njeje
Proudly powered by Blogs za Mikoa