Home » » Waliobainika kutojua kusoma, kuandika sekondari waendelea na shule

Waliobainika kutojua kusoma, kuandika sekondari waendelea na shule



Na Joachim Mushi, Korogwe

WANAFUNZI waliojiunga na masomo ya kidato cha kwanza mwaka
huu katika shule za Serikali na baadaye kubainika kuwa hawajui kusoma na
kuandika kwa ufasaha wanaendelea na masomo yao.

Uchunguzi uliofanywa na mwandishi wa habari hizi, katika
baadhi ya shule za sekondari kwa wilaya za Korogwe na Moshi Mjini umebaini
wanafunzi hao kuendelea na shule licha ya walimu kuwachuja na kutoa taarifa
sehemu husika kama walivyo elekezwa.

Akizungumza hivi karibuni katika mahojiano mjini Moshi,
Mwalimu Mkuu Msaidizi wa Shule ya Sekondari Mawenzi, Domin Kweka alisema kwa
mujibu wa vigezo vilivyotolewa na Wizara ya Elimu na Mafunzo ya Ufundi kubaini
wanafunzi wanaofaulu kujiunga na sekondari, wasio na sifa jumla ya wanafunzi
sita walibainika.

Alisema wanafunzi hao walishindwa kabisa kufanya vizuri
katika mtihani waliopewa jambo ambalo lilionesha ulakini katika kujiunga kwao
na masomo ya sekondari, japokuwa wanaendelea na shule hadi sasa.

"Sisi tuliwapata sita, hawa walikuwa hawajui kusoma na
kuandika na kutoa taarifa sehemu husika tunasubiri utaratibu mwingine...lakini
hadi muda huu wanaendelea na masomo ya kidato cha kwanza," alisema Kweka.

Aidha aliongeza kuwa tatizo hilo hujitokeza kila mwaka kwa wanafunzi
wanaojiunga na kidato cha kwanza na hadi sasa katika madarasa mbalimbali wapo
wanafunzi wasiojua kusoma na kuandika.

Alisema kwa shule hiyo ya Mawenzi kidato cha kwanza kina
wanafunzi sita wasiojua kusoma na kuandi, kidato cha pili wanafunzi sita,
kidato cha tatu wanafunzi watatu huku kidato cha nne kikiwa na wanafunzi wawili
wasiojua kusoma na kuandika.

Uchunguzi uliofanywa wilayani Korogwe pia ulibaini wanafunzi
walioshindwa kufaulu katika mchujo uliotolewa na Serikali kuendelea na masomo
ya kidato cha kwanza, licha ya shule kadhaa za sekondari kupeleka majina hayo
kwa viongozi wa idara husika.

Mwalimu Mkuu wa Shule ya Sekondari Nyerere Memorial ya
Wilayani Korogwe, Steven Killo alikiri shule yake kuwa na baadhi ya wanafunzi
kadhaa wasiojua kusoma na kuandika hata katika madarasa mengine japokuwa
hakutaja idadi.

Aidha aliongeza kuwa katika shule hiyo mchujo kwa wanafunzi
wapya waliojiunga kidato cha kwanza walibaini kuwepo kwa mwanafunzi mmoja
asiyejua kusoma na kuandika na kuwasilisha taarifa kwa viongozi wa idara ya
elimu wilaya na hakukuwa na maelekezo yoyote baada ya taarifa.

Akizungumzia suala hilo Ofisa
Elimu Taaluma, Halmashauri ya Mji wa Korogwe, Elius Mkwizu alisema hata hivyo
nia ya Serikali kuwapima wanafunzi hao haikuwa kuwarejesha nyumbani bali kujua
tatizo hilo na
kuangalia namna ya kulidhibiti.


Habari hii imeandaliwa na mtandao wa Thehabari.com (www.thehabari.com) kwa ushirikiano na HakiElimu

0 comments:

 
Supported by Tone Multimedia Company Limited
Copyright © 2012. Kilimanjaro Yetu - All Rights Reserved
Designed by Fredy Tony Njeje
Proudly powered by Blogs za Mikoa