Home » » HOTELI YA KNCU YAWAKA

HOTELI YA KNCU YAWAKA

na Rodrick Mushi, Moshi
HOTELI ya KNCU inayomilikiwa na Chama Kikuu cha Ushirika mkoani Kilimanjaro, imenusurika kuteketea kwa moto, baada ya sehemu ya majengo yake kuonekana yakiwa yameshika moto, kwa kile kinachosadikiwa kuwa ni hitilafu ya umeme.
Tukio la kuwaka kwa moto kwa hoteli hiyo kwenye baadhi ya vyumba vyake, lilianza majira ya saa 4:20 jana, hali iliyovuta umati wa watu wakishuhudia na kufanya juhudi mbalimbali za kuhakikisha kuwa jengo hilo linaokolewa.
Baadhi ya mashuhuda wa tukio hilo, walisema kuwa waliona moshi ukitokea kwenye madirisha ya vyumba vya hoteli hiyo, ambavyo vinakaliwa na watu binafsi, ikiwemo ofisi za Bumaco Insurance ambalo moja ya dirisha lake, lilionekana kutoa moshi mkubwa uliotanda jengo zima.
Mmoja wa wafanyakazi kwenye ofisi moja iliyopo kwenye hoteli hiyo ambaye hakutaka kutaja jina lake, alisema yeye alikuwa akiweka waya wa kompyuta kwenye mfumo wa umeme ambapo aliona mlipuko mkubwa ambao hakuelewa umetokea wapi.
Kwa upande wake kamanda wa polisi mkoani hapa, Robert Boaz, alikiri kutokea kwa tukio hilo na kusema moto huo uliathiri zaidi sehemu ya ofisi ya Bumaco, lakini hasara nyingine zikiwa bado hazijajulikana.
Alisema moto huo mkali ulizimwa baada ya askari wa zima moto kuwahi eneo la tukio na kufanikiwa kuuzima kabla haujasambaa jengo hilo.
Hata hivyo, alisema moto huo haukuweza kusababisha kifo, zaidi ya mfanyakazi mmoja (hajajulikana jina) kwenye ofisi ambazo ziliathiriwa na moto huo kujeruhiwa sehemu mbalimbali za mwili.
Chanzo: Tanzania Daima

0 comments:

 
Supported by Tone Multimedia Company Limited
Copyright © 2012. Kilimanjaro Yetu - All Rights Reserved
Designed by Fredy Tony Njeje
Proudly powered by Blogs za Mikoa