Home » » WASOMI WATAKIWA KUTOA MAONI YA KATIBA

WASOMI WATAKIWA KUTOA MAONI YA KATIBA

Mwandishi wetu, Kilimanjaro yetu
WASOMI hapa nchini wametakiwa kujitokeza kwa wingi kushiriki katika zoezi  la utoaji maoni ya katiba mpya, hatua ambayo itawezesha kupatikana kwa katiba ambayo itakidhi matakwa ya watanzania wote bila ubaguzi.

Rai hiyo ilitolewa na Katibu (M) vyuo vya elimu ya juu Bw. Christopher Ngubiagai wakati wa mahafali ya wanafunzi wa shirikisho la matawi ya CCM  la vyuo vikuu mkoani Kilimanjaro ambapo amesema wasomi wananafasi kubwa ya kuhakikisha inapatikana katiba nzuri.

Bw. Ngubiagai amesema katika kipindi hiki ambacho nchi imeanza mchakato wa uundwaji wa katiba mpya ni wakati mzuri na muafaka kwa wasomi kujitokeza kwa wingi kutoa maoni kutokana na kwamba wanaitambua vema katiba iliyopo kwa sasa na mapungufu yaliyopo.

Katika hatua nyingine katibu huyo amewataka vijana hao wasomi kujitokeza kugombea nafasi mbalimbali za uongozi ndani ya chama hatua ambayo itawezesha kupatikana kwa viongozi makini na wenye uchungu na nchi yao.

Awali akisoma risala ya wahitimu Bw. Francis Fumbuka amesema pamoja na jitihada mbalimbali walizonazo za kutaka kujenga na kuimarisha chama bado shirikisho hilo linakabiliwa na changamoto mbalimbali ikiwa ni pamoja na ukosefu wa ofisi ya kudumu,vyanzo vya mapato pamoja na vijana wengi kutotambulika kama wanachama mara baada ya kuhitimu vyuo.

Aidha katika risala hiyo, vijana wamewataka viongozi kukubali kukosolewa pindi wanapokosea ili kuweza  kurudisha heshima ya chama ikiwa  ni pamoja na kuendelea kuhamasisha watu wengi zaidi kujiunga na chama hicho.

Blogzamikoa

0 comments:

 
Supported by Tone Multimedia Company Limited
Copyright © 2012. Kilimanjaro Yetu - All Rights Reserved
Designed by Fredy Tony Njeje
Proudly powered by Blogs za Mikoa