Home » » POLISI YAWAGWAYA WATUHUMIWA WA MAUAJI

POLISI YAWAGWAYA WATUHUMIWA WA MAUAJI


na Charles Ndagulla, Moshi
WAFANYABIASHARA watatu ndugu wanaosakwa na Jeshi la Polisi nchini kwa tuhuma za kumteka, kumtesa na hatimaye kumuua Meneja wa baa maarufu ya mjini Moshi ya Mo-town, James John, wanapeta mitaani bila kukamatwa.
Uchunguzi uliofanywa na Tanzania Daima Jumatano, umebaini kuwa wafanyabiashara hao wakazi wa Kindi Kibosho wanaomiliki vitega uchumi kadhaa katika Jiji la Mwanza, wamekuwa wakionekana katika mitaa ya mji wa Moshi bila kificho.
Watuhumiwa hao, John Joseph Kisoka, Deo Joseph Kisoka na Lucas Joseph Kisoka mara nyingi huonekana mjini hapa na wakati mwingine katika Jiji la Mwanza ambako wanaendesha biashara zao.
James alitekwa katikati ya mji wa Moshi Juni 9 mwaka 2009 na kupelekwa zaidi ya kilometa 15 kutoka mjini hapa ambako alifungiwa kwenye nyumba moja inayodaiwa kumilikiwa na wafanyabiashara hao eneo la Kindi - Kibosho na kupewa mateso mbalimbali.
Wafanyabiashara hao wanatuhumiwa kumtesa James wakimshinikiza awataje watu waliohusika na tukio la mauaji ya mama yao mzazi, Martha Kisoka (68) aliyeuawa kikatili na watu wasiojulikana Mei mwaka 2009.
Mwaka 2007, James na wenzake wanne walihukumiwa kifungo cha miaka 14 baaada ya kupatikana na hatia ya kuvunja na kuiba nyumbani kwa kikongwe huyo, lakini mwaka 2008 waliachiwa huru baada ya kukata rufaa kupinga adhabu hiyo.
Baada ya mauaji hayo, wafanyabiashara hao walikimbia nchini na aliyekuwa Kamanda wa Polisi Mkoa wa Kilimanjaro, marehemu Lucas Ng’hoboko alitangaza kusakwa kwa watuhumwa hao ili washitakiwe.
Katika hatua nyingine, Mahakama Kuu Kanda ya Moshi, imeondoa shauri la jinai kwa kuwaachia huru washitakiwa wawili, Idrisa Hassan Munishi na John Mallya maarufu kwa jina la Small Boy waliokuwa wakituhumiwa kuhusika na mauaji ya marehemu James.
Shauri hilo la jinai namba PI 9/2009, liliondolewa hivi karibuni na Wakili wa Serikali, Theophil Mutakyawe mbele ya Jaji Mfawidhi wa Mahakama Kuu Kanda ya Moshi, Stella Mgasha.
Chanzo: Tanzania Daima

0 comments:

 
Supported by Tone Multimedia Company Limited
Copyright © 2012. Kilimanjaro Yetu - All Rights Reserved
Designed by Fredy Tony Njeje
Proudly powered by Blogs za Mikoa