Home » » ACHENI KUTOA MAONI KWA WANASIASA TU-WITO

ACHENI KUTOA MAONI KWA WANASIASA TU-WITO

Na Upendo Mosha, Moshi
WANANCHI wametakiwa kujitokeza kutoa maoni ya Katiba mpya juu ya namna ya kudhibiti vitendo vya ukiukwaji wa haki za binadamu na kuacha mara moja, tabia ya kutoa maoni juu ya wanasiasa pekee.

Afisa wa Kitengo cha Ushawishi na Utetezi wa Shirika lisilo la Kiserikali linalojishughulisha na Haki za Binadamu, Usawa wa Kijinsia na Msaada wa Kisheria (KWIECO), Hilari Tesha aliyasema hayo wakati wa kutoa mafunzo ya kisheria katika kata ya Njoro iliyopo wilayani Same mkoani Kilimanjaro.

Alisema, baadhi ya wananchi ambao hawajafahamu nini maana ya Katiba na kufikiri, wanadhani Katiba ipo kwa ajili ya wanasiasa tu.

Alisema, wanawake wengi wamekuwa wahanga wakubwa wa ukiukwaji wa haki za binadamu na kwamba, kujitokeza kwao, kutoa maoni juu ya namna ya kuthibiti vitendo hivyo.

Alisema ni muhimu kwa wanawake kujitetea katika Katiba, kwani ndio njia pekee ya kujinasua katika vitendo vya ukatili wa kijinsia vilivyoshamiri nchini.

“Wananchi wamekuwa wakijitokeza kutoa maoni yao juu ya Katiba mpya, lakini wamekuwa wakijisahau na kuona wanasiasa ndio wanaohusika zaidi,” alisema.

Akizungumza baada ya mafunzo hayo, Mwenyekiti wa Kamati ya Haki za Binadamu katika kata hiyo, Emanuel Zephania alisema, kumekuwa na vitendo vingi vya ukiukwaji wa haki za binadamu katika vijiji vya kata, hivyo na kwamba zaidi ya kesi 11 za ukatili zimeripotiwa, ndani ya miezi miwili iliyopita.

Baadhi ya wananchi, walisema kumekuwa na vitendo vingi vya ukiukwaji wa haki za binadamu na kulitaka Jeshi la Polisi kufanya doria za kila mara katika maeneo hayo, kutokana na kutishiwa kutoa habari za ukatili zinazofanywa na baadhi yao.

Walisema bado, elimu zaidi inahitajika ya haki za binadamu vijijini, kutokana na matukio mengi, yamekuwa yakitendeka vijijini.
Chanzo: Mtanzania

0 comments:

 
Supported by Tone Multimedia Company Limited
Copyright © 2012. Kilimanjaro Yetu - All Rights Reserved
Designed by Fredy Tony Njeje
Proudly powered by Blogs za Mikoa