Home » » KAGASHEKI: WANAWAKE PANDENI KILIMANJARO

KAGASHEKI: WANAWAKE PANDENI KILIMANJARO

na Asha Bani
WAZIRI wa Maliasili na Utalii, Balozi Khamis Kagasheki, amewataka wanawake kupanda Mlima Kilimanjaro kama mchango wao katika kuutangaza utalii nchini.
Aliyasema hayo jana ofisini kwake mara baada ya kukutana na Mkurugenzi Mkazi wa Shirika la Chakula Duniani (WFP) nchini Tanzania, Richard Regan, ambaye alimtembelea.
Kwa mujibu wa taarifa ya wizara hiyo iliyotolewa na Msemaji wake Mkuu, George Matiku, madhumuni ya ziara ya Regan ni kumfahamisha waziri huyo kuhusu mradi wa WFP unaowawezesha wanawake kushiriki katika shughuli za utalii hususan ya kupanda milima.
Mkurugenzi huyo alimweleza waziri huyo kuwa ifikapo Machi mwakani shirika lake litawawezesha wanawake kupanda Mlima Kilimanjaro chini ya mradi uitwao “Kutoka Mlima Everest hadi Mlima Kilimanjaro”.
Alisema chimbuko la mradi huo ni nchini Nepal mwaka 2008 ambapo baada ya kuwezeshwa wanawake 10 walipanda Mlima Everest hadi kileleni.
“Hakuna mlima mwingine kama Kilimanjaro, hivyo sharti mbinu mbalimbali zitumike, lakini mafanikio yatakuwa makubwa zaidi kama wanawake watahusika,” alisema.
Chanzo: Tanzania Daima

0 comments:

 
Supported by Tone Multimedia Company Limited
Copyright © 2012. Kilimanjaro Yetu - All Rights Reserved
Designed by Fredy Tony Njeje
Proudly powered by Blogs za Mikoa