na Rodrick Mushi, Moshi
WAKAZI wa
Manispaa ya Moshi wametofautiana kuhusu mvutano uliopo baina ya Mkuu wa Mkoa wa
Kilimanajro, Leonidas Gama, na Baraza la Madiwani wa Manispaa ya Moshi
linaloongozwa na CHADEMA.
Mvutano huo ni
ule wa mkuu wa mkoa kuzuia safari ya madiwani na watendaji kwenda Kigali,
Rwanda.
Wakizungumza
kwa nyakati tofauti jana, baadhi ya wananchi walisema hawahitaji mvutano wa
kisiasa kwani kama mkuu wa mkoa ingependeza zaidi wakashauriana kwa lengo la
kuleta maendeleo na sio kujitafutia umaarufu kupitia vyombo vya habari.
“Ukifuatilia
utagundua mkuu wa mkoa ana makosa, kwani kulikuwa kuna ubaya gani kama wangekaa
wakashauriana na kama anasema wangetumia sh milioni 200 basi angeacha waende
ndipo awashtaki kwa wananchi maana sisi ndio tuliowachagua,” alisema Peter
Anase, mkazi wa kata ya Njoro.
Alisema
kinachoonekana ni kutaka kudhoofisha baraza la madiwani ambalo linaongozwa na
upinzani, hivyo ni vema serikali ya CCM ikawaacha madiwani hao wakafanya kazi
na kama wakishindwa basi wahukumiwe kwenye uchaguzi na wananchi.
Lakini kwa
upande mwingine, wapo wananchi waliohoji kuhusiana na ahadi ambazo walitoa
madiwani wakati wa kampeni mwaka 2010 kuwa ni kuondoa safari zote ambazo si za
lazima za madiwani na watendaji kwenda nje ya nchi.
Mmoja wa
wananchi ambao hawakutaka kutaja majina gazetini alisema fedha ambazo zilikuwa
zitumike kwenye safari hiyo ni kubwa kutokana na kata wanazoongoza kuwa na
changamoto mbalimbali.
“Ukweli lazima
niseme hata kama wao wamepunguza hizi safari lakini bado kiwango cha fedha ni
kikubwa, hata kama ni bajeti ya Waziri Mkuu wao kama madiwani wana uwezo wa
kukaa na kuamua ziende kwenye kazi fulani na sio safari na ikapitishwa,”
alisema.
Mwishoni mwa
wiki iliyopita, CHADEMA ilifanya mkutano na kutoa ufafanuzi juu ya taarifa za
safari hiyo ambayo ilinukuliwa na baadhi ya vyombo vya habari kuwa ilikuwa ya
kifisadi, kitu ambacho CHADEMA ilisema huo ni mpango wa kuwachafua madiwani hao
unaofanywa na CCM kwa lengo la kuwagombanisha na wananchi.
Chanzo: Tanzania Daima
0 comments:
Post a Comment