Home » » TPC YAPINGA SUKARI KUUZWA GHALI

TPC YAPINGA SUKARI KUUZWA GHALI

na Rodrick Mushi, Moshi
UONGOZI wa Kiwanda cha Sukari cha TPC, umetoa wito kwa serikali kuangalia upya mfumo wa usambazaji sukari ambao umeelezwa kuwa na matatizo, hivyo kuchangia bidhaa hiyo kuuzwa kwa bei ya juu kwa wananchi.
Ofisa Utendaji na Utawala wa kiwanda hicho, Japhary Ally, alisema hayo mjini hapa jana na kuongeza kuwa kiwanda hicho hakikubaliani na bei ya sh 2,000 hadi 2,500 ambayo wananchi wanaendelea kuuziwa kutokana na wao kuiza kwa bei ya kawaida.
Alisema mfumo wa usambazaji ndio unaochangia kuendelea kuuzwa ghali kwa bidhaa hiyo, hivyo ni vema serikali ikachukua hatua.
Ally alisema kulingana na bei ambayo wamekuwa wakiwauzia wauzaji wa jumla kwa mfuko wa kilo 50 kwa sh 76,000 wafanyabiashara wasingepaswa kuuza bei wanayoitumia sasa.
“Serikali isipoangalia kwa umakini suala la wafanyabiashara kuendelea kuwalangua wananchi, lawama tunakuwa tunatupiwa wazalishaji kuwa ndio tunauza bidhaa hiyo ghali, lakini kwa bei wanayouza wao sisi tungepaswa kuuza mfuko sh 100,000,” alisema Ally.
Hata hivyo, aliwatupia lawama wafanyabiashara wakubwa ambao alisema wanaagiza na kuuza sukari kutoka nje ya nchi, huku wakiendelea kuihodhi inayotoka kiwandani hapo.
Alisema kiwanda hicho kilikuwa kinauza hadi tani 400 hadi 450, lakini sasa kinauza tani 200-220 kutokana na tabia hiyo ya wafanyabiashara.
Chanzo: Tanzania Daima

0 comments:

 
Supported by Tone Multimedia Company Limited
Copyright © 2012. Kilimanjaro Yetu - All Rights Reserved
Designed by Fredy Tony Njeje
Proudly powered by Blogs za Mikoa