Home » » MAJAMBAZI YAIBA SILAHA YA KIONGOZI

MAJAMBAZI YAIBA SILAHA YA KIONGOZI

Na Salome Kitomary

Kundi la watu sita wanaosadikiwa kuwa ni majambazi wamevamia nyumba ya Mwenyekiti wa Kijiji cha Chemchem kata ya Arusha Chini, wilayani Moshi na kupora bunduki aina Shortgun.

Kutokana na tukio hilo, kumekuwa na utata kwani Mwenyekiti huyo, Karibia Mmari, akisema watu waliovamia nyumbani kwake ni wafugaji jamii ya kimasai ambao wanapinga jitihada zake za kuzuia kulisha mashamba ya wakulima, huku Kamanda wa Polisi akisema imeporwa na majambazi.

Akizungumza na NIPASHE, Mwenyekiti huyo, Karibia Mmari, alisema baada ya kuvamiwa alitoa taarifa kwenye kituo cha polisi na kufungua jalada namba TU/RB/687/2012.

Alisema siku ya tukio, alipewa taarifa kuwa kundi hilo lingevamia nyumbani kwa mke mkubwa na kwamba alibadili njia na kwenda kwa mke mdogo na ndipo walipofika na kumweka chini ya ulinzi mke wake wakamtishia kwa bastola na kisha kuanza upekuzi.

Alisema walipekuwa lakini hawakuchukua kituo chochote zaidi ya bunduki hiyo huku wakitoa maneno ya vitisho kuwa watahakikisha wanamuua kwa kuwa anazuia wafugaji wasilishe mifugo yao kwenye eneo hilo.

Katika barua yake ya Septemba 15, mwaka huu, kwenda kwa Mkuu wa wilaya ya Moshi, alisema anaishi maisha ya mashaka na familia yake, na amewapa polisi majina ya watu wanaotajwa kwenye tukio hilo lakini hawajakamatwa.

Alisema licha ya kufanyika kikao cha ujirani mwema na Mkuu wa wilaya, Dk. Ibrahim Msengi, kuwataka kila upande kufuata sheria, lakini wafugaji hao kutoka vijiji vya Kiruani na Magadini wamekuwa wakilisha mifugo kwenye mashamba ya wakulima bila woga.

Kamanda wa Polisi mkoani Kilimanjaro, Robert Boaz, alisema upelelezi wa awali wa polisi unaonyesha kuwa bunduki hiyo imeibwa na majambazi na kuwaomba wananchi kutoa ushirikiano kwani itatumika vibaya ikiwa ni pamoja na kuangamiza maisha yao.
Chanzo: Nipashe

0 comments:

 
Supported by Tone Multimedia Company Limited
Copyright © 2012. Kilimanjaro Yetu - All Rights Reserved
Designed by Fredy Tony Njeje
Proudly powered by Blogs za Mikoa