Home » » WAZAZI WALALAMIKA WATOTO WAO KUSIMAMISHWA MASOMO

WAZAZI WALALAMIKA WATOTO WAO KUSIMAMISHWA MASOMO

na Rodrick Mushi, Moshi
BAADHI ya wazazi wenye wanafunzi wanaosoma katika Shule ya Wasichana ya Visitation, wamelalamikia kitendo kilichofanywa na uongozi wa shule hiyo kuwasimamisha masomo kwa mwezi mmoja wanafunzi wa kidato cha sita, huku wawili wakifukuzwa kabisa.
Wazazi hao walisema walipata barua ya kusimamishwa masomo kwa wanafunzi hao Agosti 22 mwaka huu na kuongeza kuwa wanafunzi wengine sita wametakiwa kutoendelea na masomo hadi siku ya  kufanya mtihani wao wa mwisho.
Mmoja wa wazazi wa wanafunzi hao alisema alipata barua kutoka kwa mkuu wa shule hiyo inayomilikiwa na Kanisa Katoliki, Jimbo la Moshi, kuwa wamewasimamisha masomo wanafunzi hao baada ya kukutwa na makosa yaliyochangia kuvunja sheria za shule.
“Kwa kweli kitendo kilichofanywa na uongozi wa shule hakijatufurahisha, kwani wazazi hatujashirikishwa na watoto wetu kabla ya kurudishwa walikuwa wanachapwa na kulazimishwa kuandika barua kuwa wamefanya makosa hayo,” alisema mmoja wa wazazi hao.
Walisema mpaka wanawapokea watoto wao, uongozi haujawaambia kitu kinachoeleweka na kwamba wakati mwingine uongozi wa shule na walimu hutupiana mpira kuhusu suala hilo.
Mmoja wa wanafunzi hao waliosimamishwa, alisema kabla ya kusimamishwa masomo walihojiwa na kamati ya nidhamu na kuchapwa kwa siku mbili huku wakilazimishwa kuandika barua na kukubali makosa waliokuwa wamedaiwa kufanya ya utovu wa nidhamu.
Miongoni mwa makosa yaliyoambatanishwa kwenye barua zilizotumwa kwa wazazi ni kuchangia fedha kununua simu, kusema na kusimamia uongo juu ya mwanafunzi aliyekuwa akimiliki simu waliyokutwa nayo, kuagiza vitu mbalimbali nje ya shule pamoja na wengine waliofukuzwa kuwa na makosa ya kunywa pombe na kugawa pombe.
Kwa upande wake, Mkurugenzi wa Elimu Jimbo la Moshi, Father Willium Ruaichim, alikiri kusimamishwa masomo kwa wanafunzi hao na kusema walifanya hivyo ili kutoa nafasi kwa bodi ya shule hiyo kufanya maamuzi ya makosa waliyokutwa nayo wanafunzi hao.
Chanzo: Tanzania Daima

0 comments:

 
Supported by Tone Multimedia Company Limited
Copyright © 2012. Kilimanjaro Yetu - All Rights Reserved
Designed by Fredy Tony Njeje
Proudly powered by Blogs za Mikoa