Na Mwandishi wetu,
Moshi.
SIKU chache baada ya Waziri Mkuu
Mstaafu Bw. Frederick Sumaye, kuzungumzia swala la rushwa ndani ya chaguzi za
Chama Cha Mapinduzi, (CCM), Waziri wa Afrika Mashariki, Bw. Samwel Sitta,
amekiri kuwepo hali ya rushwa ndani ya chama hicho na kusema wale
wanaosababisha hali hiyo dawa yao iko jikoni.
Bw. Sitta aliyasema hayo mjini Moshi,
mkoani Kilimanjaro, wakati akitoa salamu zake katika mkutano mkuu wa uchaguzi
wa Umoja wa Vijana wa CCM, (UVCCM), mkoani Kilimanjaro, wakati akitokea kwenye
ziara ya kikazi Taveta, nchini Kenya.
“Wana CCM tunasemwa mambo fulani fulani
na sisi kama watu wazima na wenye busara na hekima lazima tukiri na tutafute
njia ya kujirekebisha”, alisema.
Bw. Sitta alisema kuna watu ndani ya
CCM ambao wanafikiria maslahi yao binafsi na kwamba tayari wameunda mtandao wao
kwa lengo la kutafuta Urais mwaka 2015 ambapo alisema hawatafika popote.
“Huwezi kutengeneza mtandao wa kifedha
ndani ya CCM na ukashinda, chama na wanachama wake hawatakuvumilia; CCM inayo
katiba yake na ndiyo itakayotumika kuwadhibiti watu wa namna hii wakati
ukifika”, alisema.
Alisema ubaguzi ndani ya CCM unaoendelea
sasa ndani ya chaguzi CCM zinazoendelea nchini kote umetokana na wale
wanaotumia fedha zao kujitengenezea mitandao ili wajiinue wao binafsi huku
wakisahau maslahi ya chama, nchi na wananchi kwa ujumla.
“Kufikia Novemba, mwaka huu, kutatokea
mabadiliko makukbwa ndani ya chama na ambayo baadhi yenu mliochaguliwa leo
mtashiriki historia hii na baada ya hapo tutazunguka nchi nzima kuwaelezea
wananchi hatma ya nchi yetu”, alisema.
Kuhusu vijana Bw. Sitta alitahadharisha
ya kuwa ikiwa hawataenziwa kulingana na umuhimu wao kwa kupewa maisha bora CCM
na nchi kwa ujumla itayumba.
“Namna ya kuwaenzi vijana ni
kuhakikisha wanaishi maisha mazuri na marefu, si unashiba wewe tu huku
ukiwaacha wakilala njaa kisha wakichachamaa unasema hawana adabu”, alisema huki
akishangiliwa kwa nguvu na vijana hao.
Aidha Waziri Sitta alielezea
kusikitishwa kwake na baadhi ya viongozi wa kisiasa haswa wa upinzani
wanaotumia changamoto za kimaisha zilizopo kwa kuwadanganya na kuwachanganya
wananchi huku wakiwapa matumaini ya kuwapa huduma zikiwemo za bure.
“Kazi ya serikali ni kutafuta njia ya
kuwawezesha wananchi ili waondokane na umasikini, wapate mapato, walipe kodi na
mwishowe wapate huduma nzuri na si kuwaliwaza ili wabaki na umasikini wao huku
ukiwaahidi ya kuwa ukishika madaraka utawapa huduma za bure, hizo ni siasa za
kipuuzi na ambazo hazina maana"alisema.
Blogzamikoa
0 comments:
Post a Comment