MOSHI.
WATU 20 wanashikiliwa na jeshi la polisi mkoani Kilimanjaro, kwa tuhuma za kukutwa wakijihusisha na biashara ya pombe haramu aina ya Gongo,Bhangi pamoja na Mirungi.
Watu hao walikamatwa katika maeneo mbalimbali mkoani Kilimanjaro, kufuatia operesheni iliyoanzishwa na jeshi hilo kuanzia Novemba sita, kwa lengo la kukomesha biashara ya gongo na madawa ya Kulevya.
Katika Operesheni hiyo pamoja na kukamatwa kwa watu hao, pia zilikamatwa Lita 202 za Gongo,Mirungi Kg 26, Bhangi Kg 30 na mitambo Miwili ya kutengenezea Pombe haramu aina ya Gongo.
Akitoa taarifa hiyo kwa waandishi wa habari ofisini kwake kamanda wa polisi mkoani Kilimanjaro Bw. Robert Boaz, alisema kati ya watu hao 20, watu nane walikamatwa na Mirungi,sita Bhangi na wengine Sita Gongo.
Alisema uchunguzi uliofanyika umebaini kuwa watu hao wengi ni wafanyabiashara wa madawa hayo na Gongo na kwamba zoezi la opereshen litakuwa endelevu hadi uhalifu huo utakapokwisha katika mkoa wa Kilimanjaro.
Aidha alisema watu hao ambao wanafanyia biashara zao maeneo mbalimbali mkoani Kilimanjaro, watafikishwa mahakamani wakati wowote ili kujibu mashtaka yanayowakabili.
Operesheni hiyo imeanza siku chache toka jeshi hilo kutangaza madawa ya kulevya kuendelea kuwa tatizo kubwa mkoani Kilimanjaro, ambapo katika kipindi cha Januari hadi Septemba mwaka huu Jumla ya Kg. 7.787 za Cocaine na Kg. 3.779 za Heroine zilikamatwa mkoani humo.
Pamoja na Cocaine na Heroine, pia katika kipindi hicho ilikamatwa Bhangi Kg.454.94 na Mirungi Kg. 790.6 katika maeneo mbalimbali mkoani Kilimanjaro,ambapo wahanga wakubwa wa madawa hayo wanaelezewa kuwa vijana ambao ni nguvu kazi ya taifa.
0 comments:
Post a Comment