Na Florah Temba,
Moshi.
TATIZO la wahamuaji haramu kuingia nchini kinyume cha sheria limeendelea kuongezeka ambapo katika kipindi cha Julai hadi Oktoba mwaka huu, jumla ya wahamiaji haramu 328 wamekamatwa katika maeneo mbalimbali mkoani Kiliamnjaro.
Mbali na wahamiaji hao, katika kipindi cha Novemba Nane hadi Novemba 13 walikamatwa wahamiaji wengine 15 Raia wa nchini Ethiopia kwa tuhuma za kuingia nchini Kinyume cha sheria.
Hayo yalibainishwa jana na kamanda wa polisi mkoani Kilimanjaro Bw.Robert Boaz, wakati akizungumza na waandishi wa habari ofisini kwake, ambapo alisema bado uchunguzi unaendelea ili kubaini mtandao unaohusika na usafirishaji wahamiaji hao.
Alisema kati ya wahamiaji hao 328, 312 ni kutoka nchini Ethiopia, 14 ni kutoka nchini Somalia, mkenya mmoja na mmoja ni kutoka nchin Burundi.
Kamanda Boaz alifafanua zaidi kuwa wahamiaji hao walikamatwa katika maeneo mbalimbali mkoani Kilimanjaro na kwamba wananchi wamekuwa msaada mkubwa katika kuhakikisha wahamiaji hao wanakamatwa.
“Tarehe nane Novemba, mwaka huu, tulikamata wahamiaji haramu Sita eneo la Lotima Moshi vijijini,na Novemba 12, tulikamata wengine Watano eneo la Kisima Same na jana Novemba 13, mwaka huu, tulikamata wengine Wanne eneo la Chekereni Makuyuni wilaya ya Moshi na wote hawa ni Raia wa nchini Ethiopia”alisema Kamanda Boaz.
Alisema wahamiaji hao 15 wengine walikutwa wakiwa wamehifadhiwa nyumbani kwa mtu na wengine wakirandaranda mashambani kama vile hawaelewi mahali wanapokwenda.
Aidha alisema kukamatwa kwa raia hao kumetokana na ushirikiano mzuri baina ya wananchi na Jeshi la polisi, ambapo alisema wananchi wa maeneo ya mpakani wamekuwa makini na kwamba wanapowaona watu ambao wana wasiwasi nao hutoa taarifa Polisi.
“Polisi tunaendelea na uchunguzi kubaini mtandao ambao unahusika na wahamiaji haramu, lakini pia tunawashukuru wananchi kwa kutoa ushirikiano katika hili na pia katika kulinda maeneo ya mipaka yetu” alisema Boaz.
0 comments:
Post a Comment