Home » » Majambazi wapora fedha, waiba bunduki mbili

Majambazi wapora fedha, waiba bunduki mbili


MAJAMBAZI wamevamia ofisi ya Chama cha Msingi cha Lyamungu kilichopo Hai mkoani Kilimanjaro na kupora Sh milioni 11 na kutoweka na bunduki mbili aina ya short gun zinazomilikiwa na chama hicho.
Imedaiwa majambazi hao walikuwa na silaha za moto na jadi na walimteka mlinzi wa chama hicho na kumjeruhi sehemu mbalimbali za mwili wake kabla ya kufanya wizi huo.

Kamanda wa Polisi Mkoa wa Kilimanjaro, Robert Boaz, alisema tukio hilo lilitokea juzi usiku katika Kijiji cha Lyamungo ambapo watu hao walivamia ofisi ya chama hicho iliyopo chini ya KNCU na kupora fedha zilizokuwamo kwa ajili ya kununua kahawa kwa msimu wa mwaka 2013/2014 na vitu vingine ambavyo thamani yake haijajulikana.

Alisema watu hao waliiba bunduki hizo ambayo moja ilitumiwa na mlinzi wa chama hicho, Yahaya Hemed (45).

Alisema majambazi hao walimkamata mlinzi na kumjeruhi sehemu mbalimbali za mwili na kisha kuvunja mlango wa ofisi hiyo na kufanya uharibifu mkubwa wa mali zilizokuwapo ndani.

Alisema kwa sasa mlinzi huyo na watu wengine saba wanashikiliwa kwa mahojiano na aliwataka wananchi kutoa ushirikiano kufanikisha kuwapata watu waliohusika na tukio hilo na hatimaye wachukuliwe hatua za kisheria.

Chanzo: Mtanzania 

0 comments:

 
Supported by Tone Multimedia Company Limited
Copyright © 2012. Kilimanjaro Yetu - All Rights Reserved
Designed by Fredy Tony Njeje
Proudly powered by Blogs za Mikoa