Victus Kiwango, Mkuu wa Sekondari ya Tanya
Na Thehabari, Rombo
KUANZISHWA
kwa Sekondari za Kata maeneo mbalimbali nchini kulikuwa na matumaini
makubwa kwa wananchi. Maeneo mengi uitikio wa wananchi umekuwa mkubwa na
shule hizo kujengwa kwa wingi hali ambayo imegeuka kuwa mzigo tena kwa
Serikali kutokana na kuelemewa katika kuzihudumia baadhi ya shule hizi
kwa baadhi ya maeneo.
Baadhi
ya shule hizi zimekuwa zikikubwa na changamoto kadha wa kadha hivyo
kuwa kikwazo kikubwa katika kufanya vizuri kitaaluma. Uchache wa vifaa
vya muhimu vya kujifunzia na kufundishia, walimu stahili hasa wa sayansi
na uduni wa miundombinu ya kutosha ya shule imebaki kuwa changamoto
zaidi.
Kimsingi
kwa tafsiri rahisi inaonekana wazi wazi kuwa Serikali imeelemewa na
mzigo wa kuziendesha kihuduma shule hizi. Na sasa mzigo huo umeangukia
kwa walimu wakuu wanaoziongoza shule hizo.
Wilaya
ya Rombo mkoani Kilimanjaro ni miongoni mwa maeneo yaliokuwa na
muitikio mkubwa wa ujenzi wa shule hizi. Wilaya hii kwa sasa imefikisha
jumla ya Shule za Sekondari 41 za Serikali, idadi ambayo ni kubwa
ukilinganisha na hapo nyuma kabla ya zoezi la uhamasishaji wa ujenzi wa
shule hizo.
Mwandishi
wa makala haya amezungukia baadhi ya shule hizi na kufanya mahojiano na
walimu, wanafunzi, wazazi/walezi, wadau wa elimu pamoja na viongozi wa
maeneo hayo kuangalia changamoto anuai zinazo zikabili shule hizi.
Urauri
Sekondari ni miongoni mwa shule za Kata zilizoanzishwa Tarafa ya
Tarakea wilayani Rombo ikiwa ni mpango wa Serikali kuendelea kusogeza
elimu ya sekondari kwa wananchi wake. Shule hii licha ya kukabiliwa na
changamoto nyingine kadhaa, hadi sasa haina walimu wa masomo ya sayansi
kama Baiolojia, Hisabati, Kemia pamoja na Fizikia.
Sim
Silayo ni Mkuu wa Shule ya Sekondari Urauri, anakiri kuwa kukosekana
kwa walimu wa sayansi kuwafundisha wanafunzi muda wote kiutaratibu ni
miongoni mwa vikwazo vya kufanya vizuri kitaaluma kwa shule yake. Hata
hivyo anasema hali hiyo haimkatishi tamaa ya wanafunzi wake kufundishwa
masomo ya sayansi shuleni hapo.
Anasema
ili kuziba pengo la walimu wa sayansi shuleni hapo ametafuta walimu wa
muda ambao ni vijana waliomaliza kidato cha sita na wanaendelea
kumsaidia kufundisha masomo ya Fizikia, Baiolojia, Kemia pamoja na
Hisabati. Anasema vijana hao wanalipwa ujira wao na shule kwa kutumia
michango inayopatikana shuleni.
Anasema
mwitikio wa ulipaji ada wa wazazi ni mdogo na fedha zinazotolewa na
Serikali hazitoshi kuendesha shule, hivyo hulazimika kutumia mbinu
kadhaa kuchangishana na wazazi kuhakikisha wanapata chochote kusaidia
baadhi ya gharama za shule. "Shule hii ni mchapuo wa kilimo lakini
watoto walikuwa hawasomi somo hilo kutokana na kutokuwa na mwalimu
husika wa somo...juzi nimejitahidi kwa kushirikiana na wazazi tumechanga
na kumpata mwalimu wa kilimo wa muda...hapa michango ya wazazi pamoja
na fungu la taaluma limetuokoa," anasema Silayo.
Kama
hiyo haitoshi mwalimu Silayo anasema shule yake haina vitabu vya
kutosha, maktaba, maabara na changamoto ya mazingira ya kuvutia
kimiundombinu kwa wanafunzi kusoma.
Mkurugenzi Mtendaji wa Wilaya ya Rombo, Judethadeus Mboya
Hata
hivyo kilio kama hicho cha ukosefu wa walimu wa sayansi kimeangukia
tena katika Sekondari ya Holili, Wilayani Rombo. Benson Samizi ni
Mwalimu Mkuu Msaidizi wa Shule hiyo, anasema shule hiyo haina kabisa
walimu wa masomo ya sayansi na badala yake hutumia wanafunzi wa kidato
cha sita kufundisha kwa muda na uongozi wa shule kuwalipa ujira wao.
"Shule
yetu imebahatika kuwa na vitabu vya sayansi vya kutosha, lakini hatuna
kabisa mwalimu wa masomo ya Fizikia na Hisabati...pamoja na hali hiyo
ili mambo yasiwe mabaya zaidi tunakodi vijana ambao hutusaidia masomo
haya kwa muda kuwafundisha wanafunzi wetu na kulipwa na shule chochote
kinachopatikana," anasema mwalimu huyo.
Katibu
wa Chama cha Walimu (CWT) Wilaya ya Rombo, Erasmo Mwingira anasema
shule nyingi za kata zina walimu wa masomo ya sanaa zaidi na hazina
walimu wa Sayansi wa kutosha. Anaongeza kuwa licha ya Serikali kujua
tatizo hilo bado imeendelea kuwapa mitihani ya masomo ya sayansi
wanafunzi bila kujali kama wanafunzi hao wamefundishwa masomo hayo.
"...Katika
Shule nyingi zina walimu wa sanaa, walimu wengi katika shule hizi ni wa
sanaa lakini wanapokuja kumpima mtoto (mwanafunzi) anapimwa kwa masomo
ya sanaa na sayansi bila kujali kama amefundishwa kwa njia gani masomo
hayo
Mwingira
anabainisha kuwa fedha zinazotolewa kuziendesha shule hizo 'capitation'
hazitoshi na mara nyingine huwa hazifiki kwa kwa wakati shuleni hali
ambayo huwalamimu walimu wakuu kubuni mbinu mbalimbali za uendeshaji wa
shule zao, ikiwemo kuweka utitiri wa michango kwa wazazi ili kuhakikisha
mambo yanaendelea.
"Sasa
hivi shule hizi zinaendeshwa na mifuko ya walimu wakuu...'capitation'
haifiki kabisa shuleni, fedha inayowafikia ni kidogo sana na haiwezi
kuendesha zile shule, walimu wanatumia mbinu zao kuziendesha shule ndio
maana unaona michango inakuwa mingi shuleni," anaeleza Mwingira
akizungumza na mwandishi wa makala haya.
Anaongeza
kuwa licha ya serikali kusisitiza kwamba ada ya sekondari ni shilingi
20,000 kwa sasa michango katika shule hizo ni mingi kiasi cha kufikia
120,000 jambo ambalo limewafanya baadhi ya wazazi kuzidiwa na mzigo wa
michango na wengine kushindwa kabisa kuimudu. Mdau huyu wa elimu anasema
vijana wa kidato cha sita ambao hutumiwa na shule nyingi kuokoa jahazi
ya masomo ya sayansi wamekuwa wakiwakaririsha wanafunzi kujibu mitihani
na sio kuwafundisha jambo ambalo ni hatari kwa elimu ya Tanzania hapo
mbeleni.
"Kujua
kusoma na kuandika si kigezo cha kumfundisha mtu...vijana hawa wa
kidato cha sita hawana mbinu za ufundishaji wanachokifanya ni
kuwakaririsha wanafunzi. Pamoja na hayo anaishauri serikali kutojitoa
katika jukumu la kuziendesha shule za kata na kuwaachia wazazi kwani
shule hizo ziko katika hali mbaya na zinahitaji kuongezewa fedha za
uendeshaji.
Victus
Kiwango ni Mkuu wa Sekondari ya Tanya, anaishauri Serikali kuongeza
fungu la uendeshaji wa fedha shuleni kwani fedha za michango
zinazotolewa na wazazi hazitoshi kuendesha shule. Anasema shule huwa
zinakodi wanafunzi waliomaliza kidato cha sita na kuwasaidia wanafunzi
kwa muda masomo ya sayansi hivyo shule kuwa na gharama kubwa za
uendeshaji.
"Sisi
tumelazimika kuajiri kwa muda wanafunzi sita waliomaliza kidato cha
sita kufundisha masomo ya sayansi kwa fedha za shule...tunajibanabana
kwa michango pamoja na wazazi na kuhakikisha tunapata chochote kuwalipa
walimu hawa wa muda bila hivyo mambo hayaendi," alisema Mkuu Msaidizi wa
Sekondari ya Nduweni, Venance Mramba akizungumza na mwandishi wa habari
hizi.
Pamoja
na hali hiyo uchunguzi wa kina uliofanywa katika shule za Sekondari za
Tanya, Nduweni, Urauri, Holili na Ngaleku na nyinginezo za wilayani
Rombo, umebaini uwepo wa ongezeko la michango shuleni hali ambayo
imelalamikiwa na baadhi ya wazazi na wadau wa elimu wilayani
waliozungumza. Uchapaini shule ya Sekondari Tanya imefikisha jumla ya
michango sh. 115,000; mgawanyiko wake ukiwa kama ifuatavyo; Ada sh
20,000, Madawati sh 15,000, Chakula sh 60,000, Tahadhari sh 5,000,
Ulinzi 5,000, Taaluma sh 5,000 na Kitambulisho sh 5,000.
Aidha
uchunguzi zaidi umebaini shule nyingi za sekondari za kata hazina
walimu wa masomo ya sayansi jambo ambalo huwalazimisha walimu wakuu
kutafuta walimu wa kukodi hasa wanafunzi waliomaliza kidato cha sita
kuja kuwafundisha wanafunzi masomo ya sanyansi kama Hisabati, Fizikia,
Kemia, Baiolojia na mengineyo huku wakitumia mbinu anuai kukusanya
michango kuwalipa walimu hao wa kukodi.
Judethadeus
Mboya ni Mkurugenzi Mtendaji wa Wilaya ya Rombo, katika mazungumzo na
makala haya anakiri kuwepo na tatizo la upungufu wa walimu wa sayansi
katika shule nyingi za wilaya yake, hivyo walimu kulazimika kuajiri kwa
muda vijana wa kidato cha sita kusaidia wanafunzi huku jitihada
zikiendelea kufanya kukabiliana na tatizo hilo.
"Walimu
wa sayansi ni tatizo Rombo hawatoshi...mwaka huu tumejitahidi na
kuajiri takribani walimu 134 wakiwemo wachache wa masomo ya sayansi
lakini tatizo bado lipo," alisema Mboya kikilitolea ufafanuzi suala hilo
ofisini kwake wilayani Rombo hivi karibuni. Hata hivyo kiongozi huyu
mtendaji wa wilaya anasema licha ya changamoto zilizopo katika shule
hizo bado zinanafasi ya kufanya vizuri kitaaluma endapo walimu wa kuu
watajitoa kikamilifu katika kusimamia utendaji wa shughuli shuleni hapo.
"...Walimu
wakuu ndio msingi wa kufanya vibaya kitaaluma katika shule, endapo
mwalimu mkuu atatumia uwezo na ukakamavu katika kuongoza shule yake
itafanikiwa...mwalimu huyu akitumia uwezo wake kuwaongoza vizuri walimu
wengine lazima atafanikiwa na shule itafanya vizuri kitaaluma," anasema
Mboya.
Imeandaliwa na www.thehabari.com
0 comments:
Post a Comment