Home » » Fuvu la binadamu lakutwa kwenye dari

Fuvu la binadamu lakutwa kwenye dari



FUVU la kichwa cha binadamu, limekutwa likiwa limeficha juu ya dari katika nyumba ya mtu mmoja wilayani Same mkoani Kilimanjaro, kutokana na imani za kishirikina. Akizungumza na waandishi wa habari jana, Kamanda wa Polisi Mkoa wa Kilimanjaro, Robert Boaz alisema tukio hilo, lilitokea Julai 17, mwaka huu saa 8:17 mchana katika Kijiji cha Mbono.

Alisema askari waliokuwa wakisaka wauzaji wa gongo na bangi, walipekuwa nyumba ya Saidi Fundi (43) na kukuta fuvu la kichwa cha binadamu, likiwa limeficha juu ya dari katika nyumba yake.

Alisema baada ya mahojiano baina ya askari na mtuhumiwa huyo, alisema fuvu hilo ni la baba yake mzazi, Hamisi Elidina aliyefariki dunia miaka ya 1970 na kuzikwa katika eneo la Kifaru wilayani Mwanga.

Alisema mtuhumiwa huyo, alifikia uamuzi wa kufukua kaburi la baba yake kutokana na maagizo ya mizimu ya ukoo wao, kuwa akifanya hivyo atakuwa na maisha mazuri.

Alisema kutokana na tukio hilo, uchunguzi unaendelea ili kubaini kama ni kweli fuvu hilo ni la binadamu.

Alisema baada ya uchunguzi huo kukamilika, mtuhumiwa huyo atafikishwa mahakamani kujibu mashtaka yanayomkabili, kwani kukutwa na kiungo chochote cha binadamu ni kosa kisheria.
Chanzo: Mtanzania





0 comments:

 
Supported by Tone Multimedia Company Limited
Copyright © 2012. Kilimanjaro Yetu - All Rights Reserved
Designed by Fredy Tony Njeje
Proudly powered by Blogs za Mikoa