WATU wanaodhaniwa kuwa majambazi wamewateka
wafanyakazi wa Kampuni ya Ujenzi ya DOTT Service Ltd ya nchini Uganda akiwemo
mkurugenzi wake wa fedha, Shuresh Bab (45) na kuwapora fedha sh milioni 220.
Majambazi hayo ambayo idadi yake haikufahamika,
inadaiwa yalikuwa na ofisa wa polisi na baada ya tukio walifanikiwa kutokomea
kusikojulikana huku wakiwatelekeza wafanyakazi hao na gari walilokuwa wakitumia
kando ya Mto Karanga mjini Moshi.
Kamanda wa Polisi Mkoa wa Kilimanjaro, ACP Robert
Boaz, alithibitisha kutokea kwa tukio hilo na kwamba tayari hadi sasa
watuhumiwa wanne muhimu wa tukio hilo wamekamatwa wakiwa na kiasi cha fedha
ambazo zinadaiwa kuporwa.
Boaz alisema tukio hilo lilitokea juzi saa 4:00
asubuhi katika maungio ya barabara ya Arusha na Old Boma ambapo mkurugenzi
huyo, Bab, akiwa na watumishi wengine alichukua fedha sh milioni 220 toka
katika benki ya Standard Chartered tawi la Moshi.
“Watumishi hao wa Kampuni ya Dott inayojenga barabara
ya Same- Mkumbara, walikuja hapa mjini kwa ajili ya kuhamisha fedha kutoka
benki ya Standard Chartered ili wazipeleke benki nyingine ya NMB kwa ajili ya
kurahisisha malipo ya mshahara wa watumishi wao huko Same,” alisema.
Alisema wakiwa njiani na fedha hizo kuelekea
NMB katika gari aina ya Toyota Hilux Double Cabin lenye namba za usajili T
864 AZM, likiendeshwa na Wenslaus Mambo (32), walisimama kupisha pikipiki
iliyokuwa inakatisha barabara mbele yao kwenye maungio ya barabara.
Boaz alisema ghafla walijitokeza watu wawili
waliokuwa kando ya barabara wakafungua milango ya gari na kuingia ndani na
kumwamuru dereva aendeshe kuelekea eneo la Shanty Town na kwamba wakati
wakielekea, Bab alifanikiwa kuruka toka garini na kutoa taarifa polisi.
Kwa mujibu wa kamanda, hatua za haraka za
ufuatiliaji wa tukio hilo zilifanyika na kufanikiwa kulipata gari hilo likiwa
eneo la Mto Karanga pamoja na wafanyakazi hao.
“Mpaka sasa haijafahamika kama kuna silaha yoyote
ilitumika katika utekaji huo, huenda ukawa ulikuwa ni mpango, lakini
tunaendelea na uchunguzi wa kina ingawaje tunao watu wanne muhimu na majina yao
kwa sasa tunayahifadhi kwa ajili ya uchunguzi zaidi na tumefanikiwa kuokoa sh
milioni 83,” alisema Boaz.
Alipotakiwa kuthibitisha ushiriki wa ofisa wa
polisi katika tukio hilo, Kamanda Boaz hakuweza kukiri ama kukataa akisema ni
mapema sana kutaja majina ya wahusika.
Hata hivyo, Boaz alisema njia iliyotumika
kusafirisha fedha hizo ni ya kizamani sana na kwamba wahusika walikuwa wana
uwezo wa kuzihamisha kwa mawasiliano ya benki na benki.
Chanzo: Tanzania Daima
0 comments:
Post a Comment