Moshi. Askari
polisi wawili wa Kikosi cha Kutuliza Ghasia (FFU), wametiwa mbaroni kwa
tuhuma za kula njama na kushiriki katika uporaji wa Sh220 milioni za
Kampuni ya Dot Services ya mjini Moshi.
Habari
za uhakika zilisema baada ya kubanwa na makachero, askari hao
walirejesha Sh60 milioni na watuhumiwa wengine wawili ambao ni raia,
walirejesha Sh23 milioni. Askari hao ni wale walioko katika Kikosi cha
Polisi wa doria wanaotumia pikipiki na jana watuhumiwa wote walitawanywa
katika vituo mbalimbali ili wahojiwe kwa nyakati tofauti tofauti.
Habari
za kipolisi zilisema askari hao hawakwenda eneo la tukio lakini
walifahamu mpango mzima kuhusu uporaji huo uliowawezesha kupata mgawo wa
fedha hizo.
Waliotiwa
mbaroni wana vyeo vya Constable (majina tunayo) na inaelezwa kuwa tukio
hilo limewachukiza baadhi ya polisi wakidai ni kuwa mfululizo wa
matukio yanayochafua sura ya jeshi hilo.
Habari
hizo zimebainisha kuwa tukio hilo ni mpango mahususi uliowashirikisha
watu wasiopungua 10 wakiwamo baadhi ya watumishi wa Kampuni ya Dot
Services waliovujisha mpango wa kuhamisha fedha hizo.
Kulingana
na vyanzo vya habari, idadi ya walioshiriki katika mpango wa kupora
fedha hizo ni kati ya watu wanane na 10 na tayari polisi wameanzisha
msako mkali wa kuwatafuta.
Kamanda
wa Polisi wa Mkoa Kilimanjaro, Robert Boaz alikaririwa akisema kuwa
fedha hizo ziliporwa Jumanne asubuhi katika makutano ya Barabara za
Arusha na Boma mjini Moshi.
Kwa
mujibu wa Kamanda Boaz, baada ya kufika katika makutano hayo,
wafanyakazi wa Kampuni ya Dot Services waliokuwa na gari aina ya Toyota
Hilux T.864 AZM walisimama kuruhusu pikipiki ipite.
Kamanda
Boaz alisema wakati wakisubiri pikipiki ipite, ghafla walijitokeza watu
wawili wakafungua milango na kuingia ndani ya gari na kuwateka
wafanyakazi na kuwaamuru waelekee eneo la Shanty Town.
Hata
hivyo mkurugenzi wa Fedha wa kampuni hiyo ya ujenzi yenye makao yake
makuu nchini Uganda, Shuresh Bab alifanikiwa kuruka kwenye gari hilo na
kutoa taarifa polisi.
Kamanda
Boaz alifafanua kuwa msako wa kuwatafuta wahusika ulianza mara moja
ambapo polisi walifanikiwa kulipata gari hilo na wafanyakazi wakiwa
wametelekezwa mto Karanga mjini Moshi.
CHANZO; MWANANCHI
0 comments:
Post a Comment