Moshi.Malori ya nchi jirani ya Kenya
yaliyosheheni bidhaa za nafaka kutoka Tanzania, jana yalikwama kwa muda
wa saa 6 katika kituo cha mpakani cha Holili mkoani Kilimanjaro,
kutokana na mgomo wa madereva.
Mgomo kama huo unadaiwa pia kutokea upande wa
Kenya, ambako wafanyabiashara wa Kenya na Tanzania wanapinga utaratibu
wa kuruhusu kampuni moja tu kusafirisha bidhaa kwenda Kenya.
Wafanyabiashara hao wanadai kuna mipango ya
kuruhusu kampuni moja tu kununua nafaka katika Soko la Himo, Moshi
Vijijini na kuzisafirisha kwenda Kenya na kuzinyima kampuni za wazawa.
Kutokana na hoja hiyo, madereva wa malori
yaliyokuwa na namba za Kenya, waligoma kusafirisha bidhaa kwenda Kenya
huku na wale waliokuwa wakitoka Kenya nao kuungana na wenzao.
“Rais (Kikwete) ameshatangaza wakulima ruksa kuuza
mahindi kwenda Kenya, sasa huu urasimu hapa mkoani ni wa nini,
tunaambiwa sisi wazawa mwisho wetu Soko la Himo,” alidai mmoja wao.
Mkuu wa Mkoa wa Kilimanjaro, Leonidas Gama,
alipoulizwa na gazeti hili, alikiri kuzuiwa kwa malori ya Kenya katika
Kituo cha Holili, lakini akasema baada ya kuzungumza nao yameendelea na
safari.
“Sisi (Serikali) tumesema wale wote wenye vibali
vya kuleta mahindi na mazao mengine wayauze Soko la Himo halafu
wafanyabiashara wa Kenya ndiyo wanunue hapo na kupeleka kwao
Kenya,”alisema.
Gama alisema utaratibu huo utakuza uchumi wa Mkoa
wa Kilimanjaro kwa kuwa kwa ujio wa wafanyabiashara hao utafungua fursa
za kibiashara kwa wananchi wanaozunguka soko hilo.
“Wakija hapa kwetu watakula, watanunua matunda,
watakunywa kwa hiyo wataacha pesa hapa hapa mkoani kuliko utaratibu wa
kuacha soko la nafaka liwe holela,” alisisitiza Mkuu wa Mkoa.
Mgomo huo umeelezwa kuwa ni mkubwa kuwahi kutokea
katika eneo hilo la mpakani mwa nchi hizi mbili wanachama wa Jumuiya ya
Afrika Mashariki.
Serikali hivi karibuni ilitoa ruksa kwa wakulima
kuuza mahindi yao nje ya nchi, ili kuwawezesha kunufaika na kilimo cha
zao hilo na hatua hiyo ilitangazwa na Rais Jakaya Kikwete akiwaNjombe.
Chanzo;Mwanachi
Chanzo;Mwanachi
0 comments:
Post a Comment