MPANGO wa wafanyabiashara wanaosafirisha mazao kwenda Kenya wa
kutaka kuzuia magari kutoka Kenya kuingia Tanzania, juzi ulikwama baada
Jeshi la Polisi kuimarisha ulinzi katika mpaka wa Holili.
Hatua ya wafanyabiashara hao kutaka kuweka kizuizi mpakani hapo
inatokana na mgogoro uliopo sasa baina ya uongozi wa mkoa na
wafanyabiashara hao kutokana na kusitishwa kwa ghafla vibali vya
kusafirisha mazao hayo kwenda nje ya nchi.
Juzi, saa 1:30 asubuhi katika eneo hilo la mpakani kulishuhudiwa
zaidi ya malori 20 yaliyosheheni mahindi na maharage yakiwa yameegeshwa
kando ya barabara ya Holili huku askari zaidi ya saba wakiwa na silaha
za moto wakizunguka.
Tanzania Daima ilifanikiwa kuzungumza na mwenyekiti wa mawakala wa
mazao hayo, Ramadhan Lema, ambaye alikiri kuwepo kwa mgogoro baina yao
na serikali ya mkoa kutokana na hatua yake ya kusitisha ghafla vibali
vya kusafirisha mazao hayo kwenda nje ya nchi.
Mbali na kusitisha vibali hivyo pia serikali ya mkoa wa Kilimanjaro
imeiteua kampuni ya Kilimanjaro Uchumi (KUC-Ltd ) kuchukua jukumu la
usafirishaji wa mazao hatua ambayo inapingwa na wafanyabiashara hao.
Alisema endapo jambo hilo halitamalizwa haraka, watadai haki yao kwa
kuweka zuio kwa kampuni yoyote au mfanyabiashara asiruhusiwe kupita
katika mipaka hiyo ya Tanzania na Kenya hadi hapo uamuzi uliotolewa
utakapotolewa ufafanuzi wake.
“Hatutafanya vurugu wala kuandamana, isipokuwa tutatumia njia za haki
kwa kuweka pingamizi mahakamani ili haki itendeke.Kimsingi suala hili
linaweza kumalizwa na Waziri wa Kilimo, Chakula na Ushirika.
“Sisi tumepewa vibali, tunalipa mapato na tunaiingizia nchi yetu
fedha za kigeni lakini cha ajabu kampuni ya uchumi ya mkoa imepewa
jukumu hilo bila ya kutangazwa zabuni,” alisema Lema.
Alisema kutokana na hatua hiyo ya serikali ya mkoa kuweka zuio la
kuuza mazao yao Kenya hadi sasa zaidi ya tani 8,000 za mahindi na
maharage zimekwama katika mji mdogo wa Himo ukiwemo mchele tani 1,200
huku wafanyabiashara wa Kenya waliokuwa wakishirikiana na Watanzania
wakitaka kuondoa mitaji yao waliyowekeza.
Mkuu wa Mkoa wa Kilimanjaro, Leonidas Gama, alisema serikali
haijasitisha biashara hiyo kama inavyodaiwa na baadhi ya
wafanyabiashara hao wa nafaka huku akiwataka wafanyabiashara hao
kuendelea na bishara yao kama kawaida.
Naibu Waziri wa Chakula, Kilimo na Ushirika, Adam Malima, alipotakiwa
kutolea ufafanuzi sakata hilo, alisema uamuzi huo umetolewa na
serikali ya mkoa ambayo imelenga kukusanya mapato na kuongeza nguvu ya
kiuchumi kwa kuhimiza matumizi ya soko la kimataifa la nafaka lililo
katika mji mdogo wa Himo, Wilaya ya Moshi.
Chanzo;Tanzani Daima
0 comments:
Post a Comment