Home » » Mtandao wa kusafirisha wahamiaji haramu wanaswa

Mtandao wa kusafirisha wahamiaji haramu wanaswa

Mkuu wa Uhamiaji Mkoa wa Kilimanjaro, Johannes Msumile
Idara ya Uhamiaji Mkoa wa Kilimanjaro imenasa mtandao wa mawakala wa kimataifa unaohusisha vigogo wanne wa biashara ya usafirishaji wa binadamu kutoka nchi za Ethiopia na Somalia kupitia Kenya.
Mtandao huo unawahusisha raia wawili wa Burundi na mwanamke wa Kitanzania (majina tunayo).

Mkuu wa Uhamiaji mkoani humo, Johannes Msumile, alisema jana kuwa polisi kwa kushirikiana na idara yake imefanikiwa kuutibua mtandao huo baada ya kuwakamata watu hao.

Alisema mawasiliano yao ya simu yamesaidia kugundua nyendo zao na kwamba, hivi sasa wanamsaka mkazi wa Moshi (jina tunalo) akitajwa kuwa kinara wa usafirishaji wa binadamu.

Alisema bado polisi inaendelea kumsaka mkazi wa Moshi (jina tunalo), ambaye ametoroka baada ya kukamatwa kwa mtandao huo.

“Hivi sasa tunawakamata kwa wingi wahamiaji haramu kwa sababu tayari tumevunja mawasiliano yao na kinachoonekana sasa ni kwamba, wanatelekezwa huko kwenye maeneo mbalimbali baada ya kuwakamata wahusika wakuu wa biashara hiyo,” alisema Msumule.

Wahamiaji hao huvushwa kutoka Kenya na kuingia nchini kupitia mipaka ya Tarakea, Holili na Namanga na hutozwa Sh. 2,000,000 kila mmoja ili kupata ‘huduma’ hiyo kutoka kwa mawakala wa biashara ya usafirishaji wa binadamu.

Msumile alipoulizwa kuhusu hatma ya nyumba ya kulala wageni inayodaiwa kukutwa imewahifadhi wahamiaji haramu wakisubiri kusafirishwa kwenda Afrika Kusini, alisema tayari hatua za kisheria zimeshachukuliwa na serikali.

Alisema hiyo ni pamoja na kuifunga nyumba hiyo kwa muda usiojulikana kwa kuiweka chini ya uangalizi wa vyombo vya dola hadi kesi ya msingi dhidi ya watuhumiwa hao itakapomalizika.
 
CHANZO: NIPASHE

0 comments:

 
Supported by Tone Multimedia Company Limited
Copyright © 2012. Kilimanjaro Yetu - All Rights Reserved
Designed by Fredy Tony Njeje
Proudly powered by Blogs za Mikoa