JESHI la Polisi mkoani Kilimanjaro linawashikilia watu wanne
wanaodaiwa kuwa majambazi kwa kushiriki katika matukio ya unyang’anyi
na uporaji yaliyotokea hivi karibuni katika maeneo mbalimbali mkoani
hapa.
Kaimu Kamanda wa Polisi mkoani hapa, Koika Moita, aliwaambia
waandishi wa habari jana kuwa Desemba 17, majira ya saa nane mchana
katika Kata ya Kiusa Mjini, Moshi, jeshi hilo lilifanikiwa kuwatia
watuhumiwa hao mbaroni ambao hata hivyo hakuwataja majina kwa madai
kwamba upelelezi unaendelea.
Moita alisema kuwa jeshi hilo limefanikiwa kuwakamata watuhumiwa hao
baada ya kufanya msako mkali kutokana na kuongezeka kwa matukio ya
uporaji na unyang’anyi kwenye maduka makubwa, vituo vya mafuta pamoja
na makazi ya watu.
Jeshi hilo lilifanikiwa kumkamata dereva wa gari aina ya Mark II
yenye namba T 564 AUW aliyetambulika kwa jina la Nickson Urio
lililokuwa likitumiwa na wahalifu hao wa ujambazi.
“Watu hao wamekuwa wakijihusisha na ujambazi katika maeneo
mbalimbali, na sasa walikuwa wanajiandaa kufanya uhalifu sehemu
mbalimbali za mkoa huu, hivyo polisi tupo makini na tunawahakikishia
wananchi usalama, na tutaendelea kuwakamata wote wanaojihusisha na
vitendo hivi,” alisema Moita.
Aliongeza kuwa watuhumiwa walikiri kushiriki katika matukio
mbalimbali ya uporaji, na walipopekuliwa walikutwa na bunduki aina ya
short-gun ambayo imekatwa mtutu na kitako chake huku ikiwa haina namba.
Walikutwa pia na vitu mbalimbali, zikiwemo kompyuta mpakato mbili,
vibao vya namba za magari vitatu, funguo za magari, simu nane pamoja na
vocha za mitandao mbalimbali ya simu ambazo hazijajulikana thamani
yake.
Chanzo;Tanzania Daima
0 comments:
Post a Comment