Home » » MRT SACCOS yaonya wanachama wake

MRT SACCOS yaonya wanachama wake

CHAMA cha Ushirika wa Akiba na Mikopo cha walimu Moshi vijijini (MRT SACCOS) kimetoa siku 40 kwa baadhi ya wanachama wake kurejesha fedha za mikopo na wasipofanya hivyo watafungiwa kupata huduma hiyo.
Mbali na kusitishwa kwa huduma hiyo kwa wanachama hao ambao walipatiwa mikopo ya dharura mwaka 2012, pia MRT SACCOS inakusudia kuanza mikakati ya kuwafuatilia wadaiwa hao katika vituo vyao vya kazi.
Akitoa taarifa ya bodi ya uongozi katika mkutano mkuu wa 16 wa chama hicho uliofanyika katika uwanja wa michezo wa Chuo Kikuu Kishiriki cha Ushirika na Biashara Moshi (MUCCoBS), Makamu Mwenyekiti wa MRT SACCOS, Nemes Kessy, alisema chama kinakusudia kufanya hivyo baada ya kushindwa kurejesha mikopo hiyo kwa wakati.
“Baadhi ya wanachama wenye mikopo ya dharura ya mwaka 2012 au zaidi wamekuwa siyo waaminifu kurejesha fedha ofisini, hivyo ifikapo Januari 31 mwakani kama hawajarejesha fedha hizo watafungiwa huduma ya mikopo hiyo,” alisema Kessy.
Katika hatua nyingine, SACCOS hiyo imesema kiwango cha marejesho ya mikopo ya wanachama hakiendani na uwiano wa utoaji wa mikopo kutokana na sababu mbalimbali ikiwemo ile ya sheria ya utumishi.
Kwa mujibu wa takwimu, tangu kuanzishwa chama hicho mwaka 1998, mikopo yenye thamani ya shilingi bilioni 1.6, imetolewa ikiwemo ya dharura yenye thamani ya sh milioni 188.5.
Chanzo;Tanzania Daima

0 comments:

 
Supported by Tone Multimedia Company Limited
Copyright © 2012. Kilimanjaro Yetu - All Rights Reserved
Designed by Fredy Tony Njeje
Proudly powered by Blogs za Mikoa