Home » » Wataka kamati iwataje wabunge wanaohusika na ujangili

Wataka kamati iwataje wabunge wanaohusika na ujangili

Mwenyekiti wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Ardhi, Maliasili na Mazingira,  James Lembeli akiwasilisha taarifa kuhusu tathmini ya matatizo yaliyotokana na Operesheni Tokomeza Ujangili, bungeni Dodoma jana. Picha na Emmanuel Herman.
Moshi. Wananchi mbalimbali wakiwamo wasomi na wabunge, wamelitaka Bunge kuweka wazi majina ya wabunge waliotajwa kuhusika na vitendo vya ujangili wa wanyamapori.
Wakati akiwasilisha taarifa ya Kamati ndogo ya Uchunguzi ya Kamati ya Ardhi, Maliasili na Mazingira kuhusu Operesheni Tokomeza Ujangili, Mwenyekiti wake, James Lembeli alisema baadhi ya wabunge walitajwa kujihusisha na ujangili.
Akizungumza jana, Wakili wa siku nyingi nchini, Peter Shayo alisema ili Serikali na Bunge waonekane wako makini na wanachukizwa na vitendo vya ujangili ni lazima wawataje hadharani wabunge hao.
Mbunge wa Iringa Mjini (Chadema), Mchungaji Peter Msigwa alisema jana kuwa hakuona mantiki ya kamati hiyo kutowataja wabunge hao.
Mwanasayansi bingwa mtafiti, Profesa Watoky Nkya alisema: “Kamati imetumia fedha nyingi za kodi za wananchi wakijua hakuna aliye juu ya sheria. Tulitarajia kuwafahamu wote waliohusika na ujangili.”
Diwani wa Kata ya Shighati, Enea Mrutu alisema haiwezekani wabunge wawang’oe mawaziri wanne lakini miongoni mwao wapo wanaotuhumiwa kwa ujangili na kuachwa bila kutajwa.
Mbunge wa kuteuliwa, James Mbatia alisema: “Kazi yetu wabunge ni kuisimamia Serikali, kwa hiyo wale wabunge waliotajwa watajwe ili nao wawajibike ili Bunge letu liwe na nia thabiti ya kuisimamia Serikali,” alisema Mbatia.
Akizungumzia madai hayo, Lembeli alisema majina ya wabunge hao yapo kwenye viambatanisho vya ripoti yake kwa Bunge.
Chanzo;mwananchi

0 comments:

 
Supported by Tone Multimedia Company Limited
Copyright © 2012. Kilimanjaro Yetu - All Rights Reserved
Designed by Fredy Tony Njeje
Proudly powered by Blogs za Mikoa