CHAMA cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA) kimedai kuwa fedha
zinazoidhinishwa na Bunge la Bajeti la Jamhuri ya Muungano kwa ajili ya
matumizi ya kawaida na shughuli za maendeleo ya wananchi haziwafikii
wananchi ipasavyo kwa baadhi ya halmashauri, ikiwemo ya Manispaa ya
Moshi kwa mwaka wa fedha wa 2013/14.
Hayo yalibainishwa na Mkurugenzi wa Sheria wa CHADEMA, Tundu Lissu,
wakati wa mikutano ya Operesheni M4C Pamoja Daima katika mikoa ya Kanda
ya Kaskazini inayoendelea akisaidiana na Mwenyekiti wa Baraza la
Vijana la CHADEMA (BAVICHA) Taifa, John Heche.
“Nataka niulize fedha zetu tulizotenga bungeni kwa ajili ya
Halmashauri ya Moshi ziko wapi? Kila mwaka tunatenga bajeti kwa kila
halmashauri na kila mkoa na zikishatengwa zinatakiwa zipelekwe
kunakohusika na zitumike kama zilivyoelekezwa,” alisema Lissu.
Alitolea mfano bajeti iliyotengwa kwa mwaka huu wa fedha kwa matumizi
ya kawaida katika Mkoa wa Kilimanjaro ni sh bilioni 175 huku sh
bilioni 32.7 zikitengwa kwa ajili ya maendeleo katika mkoa.
Lissu alisema sh bilioni 135 zilitengwa kama ruzuku ya mishahara na
kati ya fedha hizo, Manispaa ya Moshi ilitengewa sh bilioni 16 huku
mkoa ukitengewa kiasi cha sh bilioni 17 kwa ajili ya matumizi mengineyo
na Manispaa ya Moshi ikitengewa sh bilioni 2.4.
Alisema kwa mujibu wa kitabu cha orodha ya majedwali yanayoambatana
na hotuba ya waziri mkuu, kuhusu makadirio ya matumizi ya fedha cha
mwaka 2013/2014, Mkoa wa Kilimanjaro umetengewa sh bilioni 14 kwa ajili
ya mfuko wa barabara huku halmashauri ya Manispaa ya Moshi ikitengewa
sh bilioni 3.
“Mafungu yote haya ukiwauliza madiwani zimekuja? Watakwambia
hatujaziona, kama madiwani hawajaziona zimekwenda wapi? Haya mabilioni
yanayozungumzwa kwenye hiki kitabu yamekwenda wapi? Kama ni hewa
kwanini wameyaandika, kwanini wasiseme ukweli?” alihoji Lissu.
Alisema ni vema serikali ikasema ukweli kwamba fedha hakuna kuliko
kudanganya kwa kuweka kiasi kikubwa cha fedha katika vitabu hali
inayowatia shaka wananchi ya kuwa kama fedha hizo hazikufika basi
huishia mikononi mwa mafisadi.
“Ni bora viongozi watuambie kwamba hatuna hela, kwanini wanaweka
mabilioni makubwa haya? Wanataka wamdanganye nani? Na kama ni mabilioni
makubwa namna hii wanaleta chache, tutajuaje kama hazijaibiwa?
Tutajuaje kama hizo ambazo hazikuja, hazikuja kwa sababu ya ufisadi?”
alihoji Lissu.
Alisema tabia hiyo imekuwa ikifanyika kila mwaka na kwamba ili
kuondokana na hali hiyo, ni vema wananchi wakaamua kuchagua CHADEMA
wakati wa uchaguzi, ili waweze kuona matunda ya nchi yao.
“Uchaguzi wa kata moja ya Tanzania si mdogo, kwa sababu ili
tuwashinde CCM kwenye chaguzi kubwa lazima tuwashinde kuanzia chini,
tuwashinde kwenye vitongoji, tuwashinde kwenye mitaa, tuwashinde kwenye
kata, tuwashinde kwenye majimbo na tuwashinde kwenye urais, ndiyo nchi
itakuwa salama, na wakati umefika wa kufanya hiyo kazi, tusipoifanya
CCM watatuangamiza,” alisema Lissu.
Mwenyekiti wa BAVICHA Taifa, Heche, aliitahadharisha CCM kuacha kutoa
rushwa ya mahindi kwa ajili ya chakula yanayodaiwa kupelekwa katika
Kata ya Kiboriloni kwa lengo la kuwagawia wananchi ili wawapigie kura
katika uchaguzi mdogo wa udiwani utakaofanyika hivi karibuni.
Heche aliitaka Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa nchini
(TAKUKURU) kufuatilia juu ya madai ya kuwepo kwa fedha kiasi cha sh
milioni 5.5 zilizotengwa kwa ajili ya kununulia mahindi na kisha
kuyagawa kwa wakazi wa Kata ya Kiboriloni
Chanzo;Tanzania Daima
0 comments:
Post a Comment