Home » » KINARA WA USAFIRISHAJI WAHAMIAJI ATOWEKA

KINARA WA USAFIRISHAJI WAHAMIAJI ATOWEKA


IDARA ya Uhamiaji mkoani Kilimanjaro, inamsaka kwa udi na uvumba mfanyabiashara mmoja maarufu katika miji ya Moshi na Arusha kwa tuhuma za kujihusisha na usafirishaji wa wahamiaji haramu wanaotoka katika nchi za Ethiopia na Somalia.
Uchunguzi uliofanywa na Tanzania Daima, umebaini kuwa mfanyabiashara huyo anayefahamika kwa jina maarufu la ‘Papaa’ anasakwa na maofisa wa Uhamiaji kwa zaidi ya wiki mbili sasa.
Inadaiwa kuwa mfanyabiashara huyo amekuwa akitumia fedha nyingi kuharibu mienendo ya kesi zinazohusisha kukamatwa kwa magari yanayoaminika kuwa yake pindi yanapokamatwa na wahamiaji haramu.
Akizungumza na gazeti hili hivi karibuni, Mkuu wa Uhamiaji mkoani Kilimanjaro (RIO), Johannes Msumule amekiri idara yake kumsaka mfanyabiashara huyo pamoja na mtu anayedaiwa kuwa mshirika wake aliyetajwa kwa jina moja la Dullah.
Mkuu huyo wa Uhamiaji pia amekiri kupokea taarifa kutoka kwa raia wema waliofichua ushiriki wa mfanyabiashara huyo katika biashara hiyo ya kusafirisha wahamiaji haramu, ambayo inadaiwa imekuwa ikimwingizia mamilioni ya fedha kutokana na kulipwa dola 5,000 kwa kichwa kimoja.
Desemba saba mwaka jana, wahamiaji haramu 56 walikamatwa katika Kijiji cha Jiungeni, Kata ya Ruvu, Wilaya ya Same, wote raia wa Ethiopia wakiwa kwenye gari aina ya Fuso lenye namba za usajili T 188 AYU.
Habari za uhakika zinadai kuwa baada ya gari hilo kukamatwa, mfanyabiashara huyo alijaribu bila mafanikio kumshawishi kwa rushwa mkuu wa kituo cha polisi Ruvu ili aliachilie, na baada ya juhudi zake kugonga mwamba, alitoroka kuhofia mkono wa dola.
Uchunguzi umebaini kuwa Desemba 17 mwaka juzi, raia 98 kutoka Ethiopia walikamatwa eneo la Namanga mkoani Arusha wakiwa ndani ya gari na baada ya kukamatwa, mfanyabiashara huyo anadaiwa kuvuruga mwenendo wa kesi.
Habari za kiuchunguzi zinapasha kuwa mfanyabiashara huyo amekuwa akitajwa mara kwa mara katika matukio yanayohusiana na kukamatwa kwa wahamiaji haramu, lakini kwa muda mrefu amekuwa hakamatiki na vyombo vya dola.
Mmoja wa makamishna wa Jeshi la Polisi nchini (jina tunalo), anayeshughulikia masuala ya wahamiaji haramu kwa muda mrefu, amekuwa akihoji nguvu aliyonayo mfanyabiashara huyo licha ya kufahamika, lakini amekuwa hakamatwi.
Akizungumza na Tanzania Daima hivi karibuni, kamishna huyo ambaye kitaaluma ni mwanasheria, alisema wapo wafanyabiashara ambao magari yao yamekuwa yakitumika kusafirisha wahamiaji haramu, lakini wamekuwa hawakamatwi huku akimtaja mmoja wao ambaye ni ‘Papaa’.
“Wapo wenye magari ya kusafirisha wahamiaji haramu na wanafahamika, lakini hawakamatwi. Mfano (anamtaja kwa majina yake matatu), tafadhali tuwafichueni,” unasema ujumbe mfupi wa maandishi alioutuma ofisa huyo kwenye simu ya kiganjani ya mwandishi wa habari hizi.
Mwaka 2011 mfanyabiashara huyo anadaiwa  kuwatishia waandishi wa habari mjini Morogoro kuwa atawaua kama wangeendelea kuandika habari zake, vitisho ambavyo vilitokea mara baada ya  wahamiaji haramu 98 kukamatwa huko, ambapo inaaminika kuwa gari na wahamiaji hao haramu ulikuwa ni  mzigo wake.
Chanzo;Tanzania daima 

0 comments:

 
Supported by Tone Multimedia Company Limited
Copyright © 2012. Kilimanjaro Yetu - All Rights Reserved
Designed by Fredy Tony Njeje
Proudly powered by Blogs za Mikoa