MBUNGE wa Moshi Mjini, Philemon Ndesamburo, (CHADEMA) amesema
mabaraza ya manispaa kushindwa kuwawajibisha watendaji wazembe kimekuwa
chanzo cha kuendelea kuwepo kwa ufisadi kwenye halmashauri nyingi
nchini.
Ndesamburo aliyasema hayo juzi katika kikao cha baraza la madiwani
kilichokuwa kikijadili bajeti ya mwaka 2014/15, ambapo wajumbe wa kikao
hicho walilalamikia idara ya manunuzi inayodaiwa kushamiri kwa rushwa.
Alisema kuwa wakurugenzi wengi wamekuwa chanzo cha watendaji
kuendelea kufanya vibaya, huku wakipuuza maazimio yanayofanywa na
wawakilishi wa wananchi na kushindwa kuwaletea wananchi maendeleo.
“Wakurugenzi wengi wanapofanya vibaya unakuta mabaraza ya madiwani
yanaishia kuazimia kuwafungia nje au kususia vikao lakini ukweli ni
kwamba bado wanakuwa hawajamaliza tatizo,” alisema.
Alisema kuwa kutokana na madiwani kuwa viongozi wa mabaraza wanapaswa
kuwa na mamlaka ya kuwawajibisha watendaji wababaishaji wakiwemo
wakurugenzi.
Ndesamburo hakusita kumzungumzia Mkurugenzi aliyemaliza muda wake,
Bernadette Kinabo, kuwa alikuwa mzigo, kwa kuwa alishindwa kusimamia
maazimio mengi yaliyofanywa na madiwani kwenye vikao, hivyo kushindwa
kutekelezwa.
Hata hivyo kauli hiyo ilipingwa na Mkurugenzi mpya wa manispaa hiyo, Shaaban Ntarambe, ambaye alimtetea mkurugenzi huyo.
Ntarambe alisema kuwa hakuna tofauti zozote ambazo yeye ameona
zilizokuwepo kwa mkurugenzi huyo bali alikuwa akifuata taratibu za
kisheria.
Aidha, kikao hicho kilipitisha bajeti ya sh bilioni 47.8 kwa ajili ya
utekelezaji wa shughuli mbalimbali za maendeleo kwa mwaka 2014/2015.
Chanzo;Tanzania Daima
0 comments:
Post a Comment