Moshi.Halmashauri ya Manispaa ya Moshi
inachunguza mwenendo wa vijana wanaokamata magari yanayodaiwa kuegeshwa
vibaya kutokana na malalamiko makubwa kuwa zoezi hilo linatawaliwa na
ubabe.
Meya wa Manispaa hiyo, Jaffar Michael alisema
endapo vijana hao watashindwa kutumia busara na sheria zilizopo,
halmashauri haitasita kuchukua uamuzi mgumu wa kuwaondoa kazini.
Malalamiko makubwa ni baadhi ya vijana hao
kujihusisha na vitendo vya rushwa, kuingia kwa nguvu kwenye magari
yanayodaiwa kuegeshwa vibaya na kutanguliza zaidi faini badala ya kuzuia
makosa.
Baadhi yao wamejikuta wakiambulia kipigo kutoka
kwa wamiliki wa magari pale wanapojaribu kumnyang’anya dereva funguo na
vipigo hivyo vimekuwa vikiungwa mkono na wananchi wengine.
“Suala la uegeshaji mbaya linanisumbua sana,
malalamiko ni mengi. Shida ni kwamba, hata ukileta wakala mwingine
anawatumia vijana walewale wanaolalamikiwa,” alisema Meya.
Meya alisema ingawa sheria ndogo inayosimamia
makosa hayo inataka faini iwe ni Sh50,000, lakini baadhi ya vijana hao
hutoza faini ya hadi Sh100,000 kwa wamiliki wa magari ambao ni wageni.
Mmoja wa wamiliki wa magari, Adelina Shayo maarufu
kama Mama Changbay, alilalamikia kutozwa Sh20,000 eneo la Benki ya NMB
Tawi la Nelson Mandela wakati alikuwa bado hajaegesha gari hilo.
“Nimeshuka tu kwenye gari ili niangalie kama
nimeegesha vizuri ama la ghafla wakaingia vijana kwenye gari yangu
wananiambia nimeegesha vibaya gari…nchi haiwezi kuendeshwa kwa staili
hii,” alilalamika.
Mfanyabiashara huyo aliyekuwa na gari aina ya
Toyota Spacio namba T103 CCQ alilipishwa faini ya Sh20,000 badala ya
Sh50,000 na kupewa stakabadhi ya halmashauri namba 247724 ya Januari 3.
Kamanda wa Polisi Mkoa wa Kilimanjaro, Robert Boaz
alisema ofisi yake inafahamu kuwapo kwa kero hiyo, lakini akasema
tatizo ni kugeuza faini kuwa ndiyo chanzo cha mapato ya halmashauri.
Chanzo:Mwananchi
Chanzo:Mwananchi
0 comments:
Post a Comment