Home » » Lembeli aibua machungu ya askari operesheni Tokomeza

Lembeli aibua machungu ya askari operesheni Tokomeza

Mwenyekiti wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Ardhi, Maliasili na Mazingira, James Lembeli.
 
Askari zaidi ya 2,000 wa vyombo vya ulinzi na usalama ambao walishiriki kuunda kikosi maalumu kilichoendesha Operesheni Tokomeza Ujangili, wanaidai serikali mabaki ya stahili zao kiasi cha Sh. bilioni 1.5.
Mwenyekiti wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Ardhi, Maliasili na Mazingira, James Lembeli, aliyasema hayo mjini Moshi jana wakati kamati yake ilipotembelea Hifadhi ya Taifa ya Mlima Kilimanjaro (Kinapa).

Lembeli alisema katika operesheni hiyo iliyofanyika mwa mwaka jana na baadaye kusitishwa Novemba mosi mwaka huo, serikali ilikuwa imetenga zaidi ya Sh. bilioni 3.5 kwa ajili ya kuitekeleza, lakini inashangaza kuambiwa kuwa askari waliohusika wanaendelea kusotea posho zao.

“Kusitishwa kwa oparesheni hakukumaanisha ukomo wake kwa kuwa askari waliendelea kulinda usalama wa maeneo yale na katika kazi hiyo ambayo wameifanya kwa moyo mmoja mpaka sasa, walitakiwa kulipwa posho zao, jukumu ambalo limesahaulika. Kwa hiyo kamati, inaitaka serikali kuhakikisha kwamba inalipa posho inazodaiwa na askari waliohusika katika operesheni hiyo,” alisema.

Askari walioshiriki operesheni hiyo ni wanajeshi 480 wa Jeshi la Ulinzi la Wananchi wa Tanzania (JWTZ), Polisi 440, wamo pia askari 440 kutoka Kikosi dhidi ya Ujangili (KDU), askari wa Wanyamapori kutoka Shirika la Hifadhi za Taifa (Tanapa) na Usalama wa Taifa.

Wengine ni askari 99 kutoka Wakala wa Huduma za Misitu (TFS) na askari Wanyamapori 51 kutoka Mamlaka ya Hifadhi ya Ngorongoro (NCAA).

Alisema ili kuondoa utata huo hiyo, kamati inashauri kufanyika kwa ukaguzi wa fedha hizo pamoja na serikali kutoa ufafanuzi wa fedha zilizobaki katika operesheni hiyo kwa kueleza sababu zilizosababisha

ucheleweshaji wa malipo ya askari hao wakati bajeti ya operesheni hiyo tayari ilikwishapitishwa.

Akizungumza na NIPASHE kwa njia ya simu Naibu Waziri wa Maliasili na Utalii, Mahamud Mgimwa, kuhusu madai ya Sh. bilioni 1.5 za askari hao, alithibitisha kusikia malalamiko hayo.

Alisema hawezi kuongea chochote kwa sababu kumbukumbu na taarifa za operesheni hiyo liko kwa watendaji wake wa chini.

“Ni kweli nimesikia malalamiko hayo tangu jana (juzi) na mara moja nimemwagiza Mkurugenzi wa Wanyama Pori Nchini, aniandalie taarifa zote kuhusu suala hilo ili niweze kulitolea ufafanuzi kwa sasa nitakuwa nasema uongo kwa sababu sina chochote nitafute kesho (leo),” alisema Mgimwa kwa njia ya simu.

DK. NCHIMBI AFUNGUKA
Wakati huo huo, aliyekuwa Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, Dk. Emanuel Nchimbi, amesema kuwa yeye pamoja na mawaziri wengine watatu walikubali kuwajibika kutokana na makosa yaliyofanywa na askari wakati wakiwa kwenye Operesheni Tokomeza Ujangili kutokana na kasi kubwa ya ujangili katika mbuga za wanyama unaotishia kutoweka kwa baadhi ya wanyama miaka 10 ijayo.

Dk. Nchimbi ambaye pia ni Mbunge wa Songea Mjini aliyasema hayo jana wakati akizungumza na wakazi wa Manispaa ya Songea kwenye viwanja vya Kiblang’oma kwenye maadhimisho ya miaka 37 ya kuzaliwa kwa Chama Cha Mapinduzi (CCM).

Alisema kuwa serikali ilifanya uamuzi kwamba iwasake majangili na kuwatokomeza kwa kutumia operesheni hiyo.

Hata hivyo, alisema wakati wa operesheni hiyo yalifanyika makosa na kusababisha vifo vya raia na askari hivyo zitatokea hoja za kuwataka viongozi wa kisiasa  wabebe dhamana ya askari ambao hawakutekeleza majukumu yao ipasavyo.

“Mimi na wenzangu tukatafakari kazi inayofanywa na askari wetu katika nchi hii kwani askari wanalala usiku na kung’atwa na mbu kwa ajili yetu sisi, wanapambana na majambazi kwa ajili ya kulinda raia, wanakufa wakiwa wanatulinda, majeshi yetu yanaingia vitani mara kadhaa kwa ajili ya kutetea raia wa Tanzania na matokeo yake mamia ya askari wanakufa kwa ajili yetu sisi,” alisema.

“Tunaombwa tuachie uwaziri kwa ajili yao, tunapata huzuni maana yake nini? Kwani kuna sababu ya kupata huzuni kwa sababu ya kutetea askari wetu,”  alihoji Dk. Nchimbi huku wananchi wakimshangilia.

Alieleza yeye na wenzake walikubali kwamba askari wanakufa kwa ajili ya raia, wanaumwa na mbu kwa ajili ya raia, wanaumizwa kwa ajili ya raia, wanateseka kwa ajili ya raia, hivyo wamekubali bakora zao ziwapige wao ili wawe salama na wapo tayari kuumia kwa ajili yao askari kutokana na kazi ngumu wanazozifanya.

Alidokeza kuwa katika kipindi cha miaka minane aliyopewa na Rais Jakaya Kikwete kutumikia wananchi ametimiza wajibu wake kikamilifu bila kumwangusha na hakuna mtu atakayeweza kuinuka kwa ujasiri na kusema kuwa mbunge wao (Nchimbi) amefanya kazi kizembe, alionea mtu au hakutimiza wajibu wake.

Alimshukuru Rais Kikwete kwa kumpa heshima kubwa ya kumsaidia katika kipindi cha miaka minane ya uongozi wake.

Desemba 20, mwaka jana aliyekuwa Waziri wa Maliasili na Utalii, Balozi Khamis Kagasheki alijiuzulu bungeni baada ya wabunge kushinikiza mawaziri ambao wizara zao zilihusika katika utekelezaji wa operesheni hiyo kuanchia ngazi.

Siku hiyo hiyo, Rais Kikwete aliteungua uteuzi wa mawaziri hao, Shamsi Vuai Nahodha (Ulinzi na JKT), Dk. Mathayo David Mathayo (Mifugo na Uvuvi) na Dk. Nchimbi.
CHANZO: NIPASHE

0 comments:

 
Supported by Tone Multimedia Company Limited
Copyright © 2012. Kilimanjaro Yetu - All Rights Reserved
Designed by Fredy Tony Njeje
Proudly powered by Blogs za Mikoa