Home » » Mrema asisitiza KNCU hakiidai serikali milioni 255/-

Mrema asisitiza KNCU hakiidai serikali milioni 255/-

Mbunge wa Vunjo (TLP), Dk. Augustino Mrema
 
Mbunge wa Vunjo (TLP), Dk. Augustino Mrema, ameendelea kushikilia kauli yake kuwa Chama cha Ushirika mkoa wa Kilimanjaro (KNCU) LTD hakiidai serikali Sh. milioni 255 zilizotokana na mdororo wa uchumi mwaka 2008/09.
Taarifa iliyotolewa kwa vyombo vya habari jana na Mbunge huyo, ilieleza kuwa kutokana na barua kutoka serikani inaonyesha kuwa deni hilo halipo tena.

Alisema taarifa zilizotolewa  katika baadhi ya vyombo vya habari  zimelenga kuchafua jina lake kwa kumuita muongo kwa wananchi wa Vunjo na Tanzania kwa ujumla.

Alisema kwa mujibu wa barua ya Katibu Mkuu wa Hazina, Ramadhani Khijjah, yenye kumbukumbu namba TYC/B/40/143/43 ya Aprili 27, 2011, kwenda kwa Meneja Mkuu wa KNCU, Serikali ilisitisha malipo hayo kwa sababu chama hicho kilipeleka madai hayo nje ya muda uliokuwa umewekwa na Serikali na kilijulishwa hakutakuwa na fidia yoyote itakayotolewa kwa chama hicho.

Alisema pia Waziri wa Fedha, Saada Mkuya Salum, alieleza bungeni Desemba 17, mwaka 2013, kwamba KNCU haiwezi kulipwa fedha hizo kwa sababu waliwasilisha madai yao nje ya muda uliokuwa umewekwa na Serikali.

Dk. Mrema alisema Naibu Waziri wa Fedha wakati ule, Janet Mbene, alisema takwimu zinazotokana na uchambuzi uliofanywa na Benki Kuu ya Tanzania (BoT) unaonyesha kwamba KNCU ilipata faida ya Sh. bilioni 2 wakati wa kipindi hicho cha mdororo wa uchumi, hivyo haistahili kupata fidia.

“Hivyo ni serikali ndiyo iliyosema kwamba KNCU ilipata faida ya Sh. bilioni 2 kwa kipindi hicho cha mdororo wa uchumi na siyo mimi, “ alisema Dk. Mrema. Taarifa ya KNCU ilidai kuwa kinaidai Serikali na kinastahili kulipwa Sh. milioni 255.1, kama fidia ya mdodoro wa uchumi wa mwaka 2008.

Meneja Mkuu wa KNCU, Honest Temba, alisema hatua ya Mrema  kusambaza kijitabu kwa wakulima akieleza kuwa KNCU haidai chochote Serikali, kauli ambazo si za kweli.
CHANZO: NIPASHE

0 comments:

 
Supported by Tone Multimedia Company Limited
Copyright © 2012. Kilimanjaro Yetu - All Rights Reserved
Designed by Fredy Tony Njeje
Proudly powered by Blogs za Mikoa