Home » » MAWAKALA WAPINGA MGOMO WA WAPAGAZI

MAWAKALA WAPINGA MGOMO WA WAPAGAZI

MGOMO uliotangazwa na Chama cha Wapagazi Tanzania (TPO) wa kugoma kutoa huduma kwa watalii katika Mlima Kilimanjaro na
Mlima Meru, umeanza kuwaumiza vichwa mawakala wa shuguli za utalii katika mikoa hiyo huku wakidai kuwa mgomo huo ni batili.
Mawakala hao wanaofanya shughuli za utalii katika milima hiyo mkoani Arusha, wamelazimika kutoa taarifa ya kupingana na mgomo huo kupitia Chama cha Wamiliki wa Kampuni za Utalii Kilimanjaro (KIATO).
Hata hivyo, kauli ya KIATO inatolewa wakati tayari kukiwa na tangazo la serikali namba 228 la Juni 29 mwaka 2009 likielekeza juu ya malipo ya dola 10 kwa wapagazi kwa siku kulingana na mabadiliko ya fedha za kigeni kwa siku hiyo.
Mbali na tangazo hilo pia kauli ya KIATO inapingana na Shirikisho la Mawakala wa Utalii Tanzania (TATO) ambao wanaonekana kukubaliana na madai ya wapagazi ya malipo ya si chini ya dola 10  kutokana na uthibitisho wa barua yao iliyosainiwa na Katibu Mtendaji wake, Sirili Akko, ikiwambusha juu ya tangazo hilo la serikali.
Katika taarifa yake kwa vyombo vya habari, KIATO kupitia katibu wake, Paul Mgana, bila kuonyesha mgomo huo ni batili kwa namna gani, ilikirushia shutuma chama cha wapagazi Tanzania huku ikidai kuwa ni chama kipya ambacho kimeanzishwa kikiwa na mkakati wa kuvuruga utalii wa milima.
Mgana alisema wao kama KIATO waliitisha mkutano na vyama vingine ambavyo wananchama wake wanajishughulisha na Mlima Kilimanjaro na Mlima Meru na kwamba TPO hawakutokea, licha ya kwamba walipatiwa mwaliko kwa njia ya simu.
Alisema katika kikao hicho kwa pamoja walikubaliana kila chama kikae na wanachama wake kufikisha mapendekezo ya kila upande na kuelezea umuhimu wa pande zote kuondoa jazba na kuwa na majadiliano yenye kuleta tija kwa pande zote.
"Tulikubaliana pia kile kiwango cha shilingi 10,000 ambacho kilipendekezwa na KIATO ndicho kiendelee kutumika kwa sasa kama kiwango cha chini kabisa na wenye uwezo zaidi na waliokuwa wakilipa sh 15,000 na kuendelea waendelee vile vile," alisema Mgana.
Alisema mazungumzo na vyama vingine bado yanaendelea bila uwepo wa TPO na kwamba chama hicho kinaonekana kutotaka mazungumzo huku kikilazimisha kiwango wakitakacho bila ya majadiliano na kutaka kujiendesha kisiasa.
Chanzo;Tanzania Daima
Ikiwa unatukio lolote au jambo lolote tuma kupitia Barua pepe yetu blogzamikoa@live.com au Whatsapp namba +255765056399.

0 comments:

 
Supported by Tone Multimedia Company Limited
Copyright © 2012. Kilimanjaro Yetu - All Rights Reserved
Designed by Fredy Tony Njeje
Proudly powered by Blogs za Mikoa