JESHI
la Polisi mkoani Kilimanjaro, limeungana na Idara ya Uhamiaji kumsaka
mfanyabiashara Emmanuel Kisima maarufu kwa jina la ‘Papaa’ anayetuhumiwa
kuwa kinara wa mtandao wa kusafirisha wahamiaji haramu.
Mfanyabiashara huyo kwa sasa yupo mafichoni katika moja ya majiji
hapa nchini akijaribu kukwepa mkono wa dola huku watu wa karibu naye
wakijaribu kuficha ukweli wakidai yuko nje ya nchi, lengo likiwa ni
kuvihadaa vyombo vya dola visibaini mahali alipo.
Akizungumza na Tanzania Daima mwishoni mwa wiki, Kamanda wa
Polisi Mkoa wa Kilimanjaro, Robert Boaz, alisema tayari jeshi hilo
limeanza mchakato wa kumsaka mfanyabiashara huyo ambaye amekuwa akitumia
jina la Mkuu wa Jeshi la Polisi nchini mstaafu (IGP), Said Mwema
kutekeleza uhalifu wake.
Kamanda Boaz ametoa wito kwa wananchi wenye taarifa sahihi za mahali
alipo mfanyabiashara huyo kwenda kutoa taarifa huku Idara ya Uhamiaji
nayo ikitoa rai kwa raia wema kumfichua.
Papaa anatuhumiwa kusafrisha kundi la wahamiaji haramu 56 kutoka
Ethiopia ambao walikamatwa Desemba 7 mwaka jana wakiwa ndani ya gari T
188 AYU Fuso katika Kijiji cha Jiungeni, Kata ya Ruvu, Wilaya ya Same.
Baada ya kukamatwa kwa wahamiaji hao haramu akiwamo dereva wa gari
hilo, mfanyabiashara huyo alijaribu bila mafanikio kutaka kuwahonga
maofisa wa polisi, ili waliachilie gari hilo, lakini juhudi hizo
ziligonga mwamba na ndipo alipoamua kukimbilia mafichoni.
Hivi karibuni, IGP Ernest Mangu, aliagiza Jeshi la Polisi mkoani
Kilimanjaro kumsaka na kumtia mbaroni mfanyabiashara huyo kutokaana na
kutumia vibaya jina la mtangulizi wake, Said Mwema.
Chanzo;Tanzania Daima
Ikiwa unatukio lolote au jambo lolote tuma kupitia Barua pepe yetu blogzamikoa@live.com au Whatsapp namba +255765056399.
0 comments:
Post a Comment