Home » » Wawili watiwa mbaroni kwa ‘unga’

Wawili watiwa mbaroni kwa ‘unga’

Kikosi cha Polisi cha Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Kilimanjaro (Kia), kimewakamata mkazi wa Ilala na raia wa Nigeria, kwa tuhuma za kukutwa na begi lenye kilo 4.8 za dawa zinazodhaniwa kuwa ni za kulevya.
Mkuu wa Upelelezi wa Viwanja vya Ndege Tanzania, Hamad Hamad, alisema watu hao walikamatwa jana saa 9 alfajiri wakisafiri kwenda Accra, Ghana kupitia Adis Ababa, Ethiopia.
Alisema watuhumiwa walikuwa mbioni kuondaka kwa kutumia ndege ya Shirika la Ndege la Ethiopia.
Hamad alisema Mtanzania anayeshikiliwa ana hati ya kusafiria yenye namba AD266957 na raia wa Nigeria, ana hati ya kusafiria yenye namba A04331402.
“Hizo dawa zimepelekwa kwa Mkemia Mkuu wa Serikali ili zikachunguzwe na kubaini kuwa ni aina gani,” alisema Hamad.
Hamad alisema watuhumiwa hao walitokea jijini Dar es Salaam kwenda mkoani Kilimanjaro, tayari kwa safari ya kwenda Accra.
“Huyu raia wa Nigeria, alikuwa anamsindikiza huyu mwanafunzi wa Chuo cha Bandari Dar es Salaam, wakitokea jijini Dar es Salaam halafu baadaye yeye abaki aendelee na shughuli zake,” alisema Hamad.
Hamad alisema watuhumiwa hao wako chini ya ulinzi mkali wa polisi huku upelelezi ukiendelea.
Hivi karibuni Kikosi cha Polisi cha Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Julius Nyerere (JNIA) kilikamata kilo 3.5 za dawa za kulevya aina ya heroini zikiwa zimefungwa kwenye vifurushi, zikipelekwa Monrovia, Liberia.
Chanzo;Mwananchi
Ikiwa unatukio lolote au jambo lolote tuma kupitia Barua pepe yetu blogzamikoa@live.com au Whatsapp namba +255765056399.

0 comments:

 
Supported by Tone Multimedia Company Limited
Copyright © 2012. Kilimanjaro Yetu - All Rights Reserved
Designed by Fredy Tony Njeje
Proudly powered by Blogs za Mikoa