Home » » Mahakama: Mtuhumiwa kesi ya twiga akamatwe

Mahakama: Mtuhumiwa kesi ya twiga akamatwe

Ikiwa unatukio lolote au jambo lolote tuma kupitia Barua pepe yetu blogzamikoa@live.com au Whatsapp namba +255765056399. 

Mahakama imetoa amri ya kukamatwa raia wa Pakistan, Kamran Ahmed ambaye ni mshtakiwa namba moja katika kesi ya utoroshwaji wa twiga wanne kwenda Uarabuni.
Hati ya kukamatwa mshtakiwa huyo ilitolewa jana na Hakimu Mkazi Mfawidhi wa Mkoa Kilimanjaro, Simon Kobelo baada mshtakiwa kushindwa kufika mahakamani jana bila kutoa sababu.
Amri hiyo inafuatia ombi lililotolewa na Wakili wa Serikali, Evetha Mushi baada ya mshtakiwa huyo kutofika mahakamani kwa siku ya pili mfululizo.
Wakili huyo aliiomba mahakama itoe amri hiyo ili mtuhumiwa akamatwe na kufikishwa mahakamani leo, na kama alikuwa ni mgonjwa awasilishe vyeti kuthibitisha ugonjwa wake.
Evetha alisema kitendo cha Ahmed kutofika mahakamani bila kutoa sababu zozote, kimeisababishia Serikali hasara kutokana na mawakili hao kusafiri kutoka Dar es Salaam hadi Moshi.
Hakimu Kobelo alikubaliana na ombi hilo la upande wa mashtaka na kuamuru mshtakiwa kukamatwa.
Mwezi uliopita, kesi hiyo ililazimika kuahirishwa baada ya mshtakiwa kuugua ghafla muda mfupi kabla ya kesi hiyo, inayowakabili pia Watanzania watatu, kuanza kusikilizwa.
Watuhimiwa wengine ni Hawa Mang’unyuka, Martin Kimath na Michael Mrutu ambao wote wako nje kwa dhamana.
Wanyama waliotoroshwa walikuwa na thamani ya Sh170.5 milioni na walisafirishwa kwa ndege kubwa ya Jeshi la Qatar.
Ushahidi wa awali mahakamani hapo unaonyesha kuwa wanyama hao walikamatwa katika maeneo ya Mto wa Mbu, Elboreti na Engaruka wilayani Monduli.
Chanzo;mwananchi

0 comments:

 
Supported by Tone Multimedia Company Limited
Copyright © 2012. Kilimanjaro Yetu - All Rights Reserved
Designed by Fredy Tony Njeje
Proudly powered by Blogs za Mikoa