Ikiwa unatukio lolote au jambo lolote tuma kupitia Barua pepe yetu blogzamikoa@live.com au Whatsapp namba +255765056399.
Wakazi wa vijiji vinne vinavyopakana na
Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Kilimanjaro (Kia), jana mchana walifunga
kwa muda barabara ya kutoka nje ya uwanja huo na kuzuia hali ya
sintofahamu kwa wageni.
Wananchi hao wanapinga kile wanachodai ni mpango
wa Serikali kuwapora ardhi ya vijiji vyao kwa madai kuwa baadhi yao
wamevamia kwenye maeneo yanayomilikiwa kihalali na Kia.
Hata hivyo, Polisi wa Kutuliza Ghasia (FFU)
walifanikiwa kuwashawishi wananchi hao, wengi wao wakiwa wanawake wa
kabila la Wamasai, kufungua barabara hiyo na kukusanyika pembezoni mwa
barabara.
Tukio hilo lilitokea saa 9:00 mchana baada ya
wananchi hao kushindwa kuafikiana katika kikao kilichoshirikisha
wanavijiji wa Sanya Stesheni, Tindigani, Mtakuja na Majengo.
Kamanda wa Polisi Mkoa Kilimanjaro, Robert Boaz
jana alilithibitishia gazeti hili kuhusu wananchi hao kufunga barabara
kwa muda, lakini akasema polisi waliokwenda eneo hilo wamedhibiti hali
hiyo.
“Ni kweli kuna wananchi walifunga barabara, lakini
tumezungumza nao na wameifungua kwa hiyo hali sasa ni shwari na magari
yanapita kama kawaida,” alisema Boaz.
Boaz alisema KIA ilipimwa mwaka 1989, lakini
wakati huo tayari kulikuwa na vijiji vilivyoandikishwa na baadhi ya
wananchi waliingia hadi eneo la uwanja huo.
“Kumekuwa na jitihada za viongozi kutatua mgogoro
huu na wiki mbili zilizopita Mkuu wa Mkoa (Leonidas Gama) na kamati
nzima ya ulinzi na usalama tulikwenda kuzungumza nao,” alisema.
Kwa mujibu wa Kamanda Boaz, katika kikao hicho
hawakufikia muafaka na ndipo baadhi yao walipohamasishana kwenda kufunga
barabara ya kwenda KIA hadi polisi walipowaondoa.
Chanzo;Mwananchi
0 comments:
Post a Comment