Ikiwa unatukio lolote au jambo lolote tuma kupitia Barua pepe yetu blogzamikoa@live.com au Whatsapp namba +255765056399.
Kamishna Msaidizi (ACP) Duan Nyanda ameieleza mahakama kuwa
mshtakiwa Samwel Saitoti alimpiga risasi ya kichwa Konstebo Michael
Milanzi na kufumua ubongo wake.
Nyanda, ambaye pia ni Mkuu wa Upelelezi wa Makosa
ya Jinai (RCO) Mkoa wa Arusha ndiye aliyeandika maelezo ya onyo (caution
statement) ya mshtakiwa huyo ambaye ni raia wa Kenya.
“Aliniambia yeye (Saitoti) ndiye alimpiga PC
Milanzi risasi ya kichwa ikafumua ubongo na wenzake walikuwa na kazi ya
kumdhibiti yule polisi mwingine aliyekuwa lindo na marehemu,” alisema.
Siku ya mauaji hayo Julai 11,2007 yaliyoambatana
na uporaji wa Sh.239 milioni mali ya Benki ya NMB Tawi la Mwanga,
Milanzi alikuwa lindoni na polisi mwenzake, PC. Naftal Asher Magoma.
Akitoa ushahidi wake mbele ya Jaji Kakusulo Sambo,
Ijumaa iliyopita ACP Nyanda alisema Saitoti alimweleza kuwa baada ya
kumuua, alimwamuru PC Magoma kulala juu ya mwili wa mwenzake.
“Wakati namuhoji aliniambia biashara ya kwenda
kupora benki ilishirikisha Watanzania na kwamba baada ya mipango
kukamilika walitumia magari ya wizi kwenda kupora na kufanya
mauaji,”alisema.
Akiongozwa na Wakili wa Serikali,Stella Majaliwa
kutoa ushahidi wake, Nyanda alisema mshtakiwa huyo alimweleza kuwa,
baada ya mauaji hayo yeye alichukua bunduki Ya marehemu aina ya SMG.
Hata hivyo Jaji Sambo alikataa kupokea maelezo ya
mshtakiwa huyo ili yawe kielelezo katika kesi hiyo inayovuta hisia za
wengi, kutokana na kubainika yalichukuliwa nje ya muda ulioruhusiwa
kisheria.
Jaji Sambo alisema, sheria inataka maelezo ya
mtuhumiwa yachukuliwe si zaidi ya saa nne tangu kukamatwa kwake na
endapo muda huo utapita, ofisa wa Polisi ataongeza muda wa saa nane.
Alisema katika kesi hiyo, mshtakiwa alikamatwa
Julai 20,2007 na kusafirishwa hadi Moshi siku hiyo hiyo lakini maelezo
yake yakachukuliwa saa 4:00 asubuhi ya Julai 22 ikiwa ni siku mbili
baadaye.
Wakati huo huo, Shahidi wa 10, Mrakibu wa Polisi
(SP) Zakaria Benard alidai, Saitoti na mshtakiwa wa pili, Peter Kimani
pia ni raia wa Kenya walitambuliwa katika gwaride la utambulisho.
Akitoa ushahidi wake kwa kuongozwa na wakili wa
Serikali, Ladslaus Komanya, shahidi huyo alidai kati ya mashahidi 10
walioitwa katika gwaride hilo lililofanyika Agosti 1,2007, mashahidi
tisa waliwatambua washtakiwa hao.
Chanzo;Mwananchi
Chanzo;Mwananchi
0 comments:
Post a Comment