Ikiwa unatukio lolote au jambo lolote tuma kupitia Barua pepe yetu blogzamikoa@live.com au Whatsapp namba +255765056399.
Waziri wa Kilimo, Chakula na Ushirika, Christopher Chiza amepiga
marufuku mtindo wa kuchumbia mazao shambani akisema kufanya hivyo ni
kumnyima mkulima kipato anachostahili.
Alisema hayo mwishoni mwa wiki alipokuwa akikagua
eneo linalotarajiwa kujengwa soko la kimataifa huko Njiapanda Himo,
mkoani Kilimanjaro.
Akizungumza na wafanyabiashara wa eneo hilo, Chiza
alisema ni marufuku kwa mtu yeyote kuchumbia mazao yakiwa shambani
kwani inawezekana mazao hayo yakazidi kiwango cha fedha alizopewa.
Aidha, alisema mtindo huo unainyima Serikali mapato kwani baadhi wanapovuna hupitisha njia za panya.
Waziri Chiza alisema hayo baada ya mfanyabiashara,
Gabriel Emmanuel anayefanya shughuli zake katika Ghala la Himo
linalohifadhi mahindi na maharagwe kumlalamikia kuwa wafanyabiashara
kutoka Kenya wanawazidi kete.
Alimweleza waziri kuwa wafanyabiashara hao wananunua mazao kwa wanavijiji kabla hayajavunwa.
Waziri aliupongeza uongozi wa Wilaya ya Rombo
hususan eneo la Tarakea kwa ukusanyaji wa mapato ambao alisema umepanda
kutoka Sh2 milioni hadi kufikia Sh4.5 milioni mwaka huu.
Chanzo:Mwananchi
Chanzo:Mwananchi

0 comments:
Post a Comment