Ikiwa unatukio lolote au jambo lolote tuma kupitia Barua pepe yetu blogzamikoa@live.com au Whatsapp namba +255765056399.
WASHITAKIWA wa kesi ya kusafirisha wanyama hai zaidi ya 100
wakiwamo twiga na ndege wa aina mbalimbali kwenda Qatar wanapandishwa
mahakamani kwa mara nyingine tena jana katika Mahakama ya Hakimu Mkazi
Moshi.
Kesi hiyo ambayo inafika mahakamani hapo kwa ajili ya kutajwa,
inawakabili washtakiwa wanne akiwamo raia wa Pakistan, Kamran Ahmad,
ipo katika hali ya sintofahamu baada ya kuahirishwa mara kadhaa baada ya
mshtakiwa huyo kutofikishwa mahakamani hapo bila taarifa yoyote.
Machi 25, mwaka huu kesi hiyo iliahirishwa baada ya mshtakiwa huyo
pamoja na wakili wake, Edmund Ngemela, kutofika mahakamani bila
taarifa.
Kesi hiyo inayosikilizwa mbele ya Hakimu Simon Kobelo, ipo katika
hatua ya ushahidi kwa upande wa Jamhuri, imesimama mara kadhaa baada ya
mshtakiwa kutofika mahakamani kutokana na sababu mbalimbali ikiwamo
kuugua.
Machi 24, upande wa Jamhuri uliomba kupewa hati ya kukamatwa
mshtakiwa huyo, lakini haikufanikiwa huku pia wakili wa mshtakiwa
huyo, Ngemela naye hakufika mahakamani bila kuwapo kwa taarifa.
Katika kesi hiyo, mawakili wa upande wa Jamuhuri, Evetha Mushi na
Steven Mwanasenjele, walidai mshtakiwa huyo anaisababishia Jamhuri
hasara kwa kuita mashahidi na kuwarejesha bila kutoa ushahidi.
Katika hatua nyingine upande wa Jamhuri umeiomba mahakama kutoa hati
ya kuitwa kwa wadhamini wa mshtakiwa huyo kutokana na mwenendo wa sasa
wa mshtakiwa kutokufika mahakamani huku kukikosekana kwa taarifa rasmi.
Baada ya kutajwa jana, kesi hiyo itasikilizwa kuanzia Mei 6 na 7 mwaka
huu, ambapo upande wa Jamhuri utaendelea kuleta mashahidi.
Washtakiwa wengine katika kesi hiyo ni Mkurugenzi wa Kampuni ya Osaka
Traders, Hawa Mang’unyuka, Ofisa Mifugo wa shamba la wanyama, Martin
Kimath na Ofisa Usalama wa Kadco, Michael Mrutu.
Washtakiwa wote wanakabiliwa na mashtaka mbalimbali ya uhujumu uchumi
ikiwamo la kusafirisha wanyama hai zaidi ya 100 wakiwamo twiga wanne
na ndege aina mbalimbali kwenda Doha, Qatar na kuisababishia serikali
hasara ya sh milioni 170.5.
Chanzo:Tanzania Daima
0 comments:
Post a Comment