Home » » Polisi wanne mbaroni kusafirisha wahamiaji haramu

Polisi wanne mbaroni kusafirisha wahamiaji haramu

Ikiwa unatukio lolote au jambo lolote tuma kupitia Barua pepe yetu blogzamikoa@live.com au Whatsapp namba +255765056399. 
Mkuu wa Mkoa wa Kilimanjaro, Leonidas Gama.
 
Jeshi la Polisi mkoa wa Kilimanjaro, limeingia katika kashfa baada ya askari wake kutuhumiwa kuwaingiza na kuwasafirisha wahamiaji haramu 47 kutoka Ethiopia.
Kutokana na kashfa hiyo, Mkuu wa mkoa huo, Leonidas Gama, ameingilia kati na kuagiza askari hao wa Kituo cha Holisi cha Himo wanaodaiwa kuhusika katika tukio hilo lililotokea Mei 02, mwaka huu, eneo la Chekereni, kuchukuliwa hatua za kisheria.

Gama ambaye pia ni Mwenyekiti wa Kamati ya Ulinzi na Usalama Mkoa wa Kilimanjaro na Mkuu wa Upelelezi mkoa, Ramadhani Moita, wamethibitisha kuhojiwa kwa askari kadhaa wa Kituo cha Polisi Himo na kwamba mahojiano yanaendelea.

Habari zinaeleza kuwa, wahamiaji hao walitoa Sh. milioni 47 kwa wakala wao ili awahakikishe njia inakuwa salama kwao hadi wanavuka vizuizi vyote vya Tanzania hadi wanaingia Malawi.

Hata hivyo, majina ya askari wanne waliohojiwa tunayahifadhi kwa sasa.

Alipoulizwa kuhusiana na tukio hilo kwa niaba ya Kamanda wa Polisi Mkoa wa Kilimanjaro, Robert Boaz, RCO, Moita alisema hawezi kulizungumzia kwa undani kwa kuwa wanaolalamikiwa na kuchunguzwa ni askari wake na kwamba agizo la kuwahoji limetolewa na mkuu wa mkoa.

Mkuu wa Mkoa, Gama alithibitisha kutokea kwa tukio hilo na kusema kuwa anao ushahidi wa kutosha unaoonyesha kuwa askari wa kituo cha Himo walikuwa wakiwasindikiza wahamiaji hao haramu.

Habari kutoka eneo la tukio walilokamatiwa wahamiaji hao, Chekereni zimeeleza kuwa Waethiopia hao walikuwa wakipatiwa ulinzi na askari mgambo waliokuwa wameahidiwa kupatiwa Sh. milioni 10 kutoka kwa wakala wao kama wangeondoka salama.

Imedaiwa kuwa wakati wakiwa katika maandalizi ya kupanda lori aina ya Fusso ndipo polisi walipotokea na kumkamata wakala wao na kuwaweka chini ya ulinzi wahamiaji hao ndipo mgambo hao walipokasirishwa na kitendo hicho.

Baadhi ya wananchi walioshuhudia tukio hilo, walisema wananchi wengi walijaa eneo la tukio na mgambo ambao walikasirishwa na kitendo cha polisi kuwatibulia mpango wao na ndipo walipoamua kumpigia simu mkuu wa mkoa wakimueleza kuwa polisi wanasindikiza wahamiaji haramu.

Mashuhuda hao walisema kuwa baada ya kupata habari hizo, mkuu wa mkoa alimpigia simu kamanda wa polisi mkoani hapa usiku huo saa tano na kumtaka ahakikishe wahamiaji hao wanafika kituo cha polisi kwa kuwa anazo taarifa za askari kutaka kuwatorosha.

Hivi karibuni, Waziri wa Mambo ya Ndani, Mathias Chikawe, akihitimisha bajeti yake ya mwaka 2014/15, alisema Mkoa wa Kilimanjaro umefanya vizuri katika kukabiliana na wahamiaji haramu kwa Kamati ya Ulinzi na Usalama ya mkoa kuwa na mikakati ya pamoja iliyowezesha mawakala na wahamiaji wanakamatwa kwa urahisi.

Aidha, Chikawe aliitaka mikoa mingine kuiga mfano wa mkoa huo ili kuhakikisha biashara hiyo inamalizwa na nchi kuacha kugeuzwa kichochoro cha kupitishia wahamiaji haramu na kwamba mkoa wa Kilimanjaro katika eneo la mpaka wa Kenya na Tanzania lilikuwa na kasi kubwa ya wahamiaji haramu kupita, lakini baada ya serikali kujipanga hali imebadilika.
CHANZO: NIPASHE

0 comments:

 
Supported by Tone Multimedia Company Limited
Copyright © 2012. Kilimanjaro Yetu - All Rights Reserved
Designed by Fredy Tony Njeje
Proudly powered by Blogs za Mikoa