Home » » TAKUKURU YABAMBA WATANO TANESCO

TAKUKURU YABAMBA WATANO TANESCO

Ikiwa unatukio lolote au jambo lolote tuma kupitia Barua pepe yetu blogzamikoa@live.com au Whatsapp namba +255765056399. 

WAFANYAKAZI watano wa Shirika la Ugavi wa Umeme Tanzania (Tanesco), wanashikiliwa na Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (Takukuru) mkoani Kilimanjaro kwa tuhuma za kuomba na kupokea rushwa ya sh 400,000.
Wafanyakazi hao ambao ni vibarua wanadaiwa kwenda nyumbani kwa Baltazar Ally, mkazi wa Shanty town mjini hapa kwa lengo la kukata umeme kwa madai kuwa alikuwa akidaiwa na shirika hilo.
Kwa mujibu wa majirani wa Ally ambao hawakupenda kutajwa majina yao gazetini, vibarua hao wa kitengo cha usomaji mita, walifika katika nyumba hiyo saa mbili asubuhi na kumkuta Ally akijiandaa kutoka kuelekea ofisini kwake.
Inadaiwa kuwa baada ya vibarua hao kufika, walilazimika kuruka geti ambalo muda wote lilikuwa limefungwa kisha wakaingia ndani na kuanza kutizama nyaya za umeme namna zilivyounganishwa.
Ally aliliambia Tanzania Daima kuwa baada ya kuingia ndani, watu hao waliendelea na ukaguzi hadi katika mita ndipo walipogundua kuwa imechezewa na kumtaka atoe sh milioni moja ili wasikate umeme.
Ally alisema hata hivyo aliwaeleza kuwa hana uhakika juu ya madai ya kuchezewa kwa mita hiyo na kwamba fedha hizo hana, na hata angekuwa nazo asingeweza kuwapatia ndipo wakaamua kuondoka.
Alisema Mei 31, wafanyakazi hao walirudi kwa mara nyingine na kumuomba awape sh laki nne ili wasimkatie umeme na alipokataa
waliukata ndipo alipokwenda kutoa taarifa Takukuru.
Meneja wa Tanesco mkoani Kilimanjaro, Martin Kasyanju, alithibitisha kukamatwa kwa wafanyakazi wake, huku akisema tayari wamewafukuza kazi watatu kati yao.
Kamanda wa Takukuru Mkoa wa Kilimanjaro, Lawrence Swema hakupatika kuzungumzia tukio hilo.
Chanzo:Tanzania Daima 

0 comments:

 
Supported by Tone Multimedia Company Limited
Copyright © 2012. Kilimanjaro Yetu - All Rights Reserved
Designed by Fredy Tony Njeje
Proudly powered by Blogs za Mikoa