Home » » SINA MPANGO KUACHIA JIMBO LA VUNJO 2015- MREMA

SINA MPANGO KUACHIA JIMBO LA VUNJO 2015- MREMA

Ikiwa unatukio lolote au jambo lolote tuma kupitia Barua pepe yetu blogzamikoa@live.com au Whatsapp namba +255765056399. 
Mbunge wa Vunjo (TLP), Augostino Mrema
Mbunge wa Vunjo (TLP), Augostino Mrema, amesema hana mpango  wa kustaafu nafasi aliyonayo kwa kuwa bado hajamalizia miradi mbalimbali ya wananchi aliyoianzisha tangu alipochaguliwa mwaka 2010.
Mrema akizungumza jana jijini Dar es Salaam katika ofisi za gazeti hili, alisema bado anahitaji muda ili aweze kukamilisha miradi hiyo.

Alitaja baadhi ya miradi hiyo kuwa ni pamoja na ujenzi wa soko kubwa la kisasa eneo la Himo na kuwasaidia vijana kujiajiri na kuondokana na kukaa vijiweni na kunywa pombe ya Mbudimbudi.
Alisema tangu achaguliwe amefanya mambo mengi yakiwamo ya ujenzi wa barabara, uwekaji wa umeme, ajira kwa vijana pamoja na kutatua kero ya maji iliyokuwa inawakabili wananchi.

Alitaja baadhi ya barabara alizozipigania na kuhakikisha zinajengwa kuwa ni pamoja na Marangu mtoni hadi Kilema sokoni, Kawawa hadi Nduoni, Kilema hadi  Pofo na  Uchira hadi Kisomachi.

Aidha, alitaja miradi mingine aliyoibuni na kuisimamia kuwa ni pamoja na kilimo cha umwagiliaji katika eneo la Rauya, Sembetini na Matara kwa lengo la kuwasaidia wapiga kura wake kujiajiri.

Kuhusu umeme, Mrema alisema wananchi wengi wa Kahe Mashariki, Magharibi, Uchira, Makuyuni na Mwika Kusini wamepatiwa nishati hiyo.

“Nimefanya mambo mengi tangu nikiwa Mbunge wa Moshi Vijijini, hivyo lazima mchango wangu nilioutoa Vunjo na maeneo mengine ya nchi uheshimiwe,” alisema Mrema.

Alimpongeza Rais Jakaya Kikwete kwa kusikiliza kilio chake na kumsaidia kutekeleza miradi mbalimbali jimboni kwake.
SOURCE: NIPASHE

0 comments:

 
Supported by Tone Multimedia Company Limited
Copyright © 2012. Kilimanjaro Yetu - All Rights Reserved
Designed by Fredy Tony Njeje
Proudly powered by Blogs za Mikoa