Home » » MWENYEKITI KITONGOJI ASAKWA KWA KUMILIKI SHAMBA LA BANGI

MWENYEKITI KITONGOJI ASAKWA KWA KUMILIKI SHAMBA LA BANGI

Ikiwa unatukio lolote au jambo lolote tuma kupitia Barua pepe yetu blogzamikoa@live.com au Whatsapp namba +255765056399. 
  Kilo 30 zakutwa nyumbani kwake
Kamanda wa Polisi mkoa wa Kilimanjaro, Robert Boaz
Jeshi la Polisi mkoani Kilimanjaro linamsaka Mwenyekiti wa serikali ya kitongoji kimoja katika kata ya Kahe, wilaya ya Moshi kwa tiketi ya CCM, ambaye ametokomea kusikojulikana baada ya wananchi kufichua shamba la bangi lenye ukubwa wa robo ekari analomiliki.
Mbali ya shamba hilo kugunduliwa, nyumbani kwa kiongozi huyo polisi pia walikamata kilo 30 za bangi, ambazo zilikuwa mbioni kusafirishwa  kwenda kuuzwa katika maeneo mbalimbali nchini.

Kamanda wa Polisi mkoa wa Kilimanjaro, Robert Boaz, jana alisema makachero wa jeshi hilo wanamtafuta kwa udi na uvumba mwenyekiti huyo, ambaye amekimbia baada ya kubaini anatafutwa kwa kosa la kulima bangi na kuhifadhi dawa hizo za kulevya nyumbani kwake kinyume cha sheria za nchi.

“Bado tunamtafuta huyu mwenyekiti lakini pia katika msako ulioendelea siku hiyo pia tulimbaini mkulima mwingine ambaye ana shamba la bangi robo ekari katika kijiji cha Kisange Sangeni, kata ya Kahe. Hawa wote wawili wamepanda na kustawisha bangi katikati ya shamba la mahindi,” alisema.

Kamanda Boaz aliwataka wakazi wa mkoa huo kuendelea kutoa taarifa za uhalifu bila ya woga wanapomtilia shaka mtu yeyote kuhusu mwenendo wake. 

 NIPASHE ilimtafuta kwa njia ya simu Katibu wa Chama cha Mapinduzi (CCM) Mkoa wa Kilimanjaro, Deogratius Rutta, kwa ajili ya kutaka kujua msimamo wa chama chake kuhusiana na madai hayo dhidi ya kada wake, ambapo alisema ni jambo la kusikitisha.

“Nimepokea kwa masikitiko makubwa taarifa hiyo lakini kwa sasa nipo mkoani Morogoro kwa mapumziko mafupi ya sikukuu ya Idd el Fitri.

Nipe muda niwatafute wasaidizi wangu ili wanipatie taarifa za kina na Mwenyezi Mungu akipenda kesho au keshokutwa nitakuwa Moshi kwa ajili ya kuendelea na kazi za chama, tuwasiliane,” alisema na kukata simu.
CHANZO: NIPASHE

0 comments:

 
Supported by Tone Multimedia Company Limited
Copyright © 2012. Kilimanjaro Yetu - All Rights Reserved
Designed by Fredy Tony Njeje
Proudly powered by Blogs za Mikoa