Home » » TUGHE YADAI KUTORIDHISHWA NA UTENDAJI WA NSSF KILIMANJARO

TUGHE YADAI KUTORIDHISHWA NA UTENDAJI WA NSSF KILIMANJARO

Ikiwa unatukio lolote au jambo lolote tuma kupitia Barua pepe yetu blogzamikoa@live.com au Whatsapp namba +255765056399. 
Shirika la Mfuko wa Hifadhi ya Jamii (NSSF)
Chama cha Wafanyakazi wa Serikali Kuu na Afya (Tughe), kimesema hakiridhishwi na utendaji wa Shirika la Mfuko wa Hifadhi ya Jamii (Nssf) mkoani Kilimanjaro kutokana na kushindwa kuzibana taasisi zinazoshindwa kupeleka michango ya wafanyakazi wao. 
 
Ilizitaja taasisi hizo kuwa ni Mawenzi, Polisi na idara ya Mahakama.
Mjumbe wa Baraza Kuu la Shirikisho la Vyama vya Wafanyakazi nchini (Tucta), Gresta Sodoka, alisema jana kuwa kusuasua kwa ufuatiliaji wa malalamiko ya wanachama wake, kumekifanya chama hicho kuunda kamati maalumu ya mkoa kwa ajili ya kuibana Nssf ieleze hatma ya waajiri sita ambao hawajapeleka michango kwenye mfuko huo.
 
“Kikosi kazi cha ufuatiliaji cha TUGHE kilichoundwa, tayari kimekutana na meneja wa Nssf mkoa wa Kilimanjaro ili atoe ufafanuzi wa mambo yanayolalamikiwa na baadhi ya wanachama wake, ikiwamo waajiri kutopeleka michango na madai ya kuwapo kwa lugha isiyopendeza dhidi ya wanachama.
 
Ametuelewa na tumempa muda wa kufutilia madai yetu,”alisema Sodoka.
Alisema ili kukomesha malalamiko ya wafanyakazi dhidi ya shirika hilo wanaolalamikiwa ni vyema Nssf ikaangalia uwezekano wa kufunga kamera maalumu (CCTV) ili kufuatilia nyendo zao.
 
Awali, Katibu wa TUGHE mkoani hapa, Simon Msuya, akizungumza katika kikao hicho aliwataja waajiri ambao hawapeleki Nssf baadhi ya michango ya wafanyakazi wao kuwa ni Hospitali ya Mkoa ya Mawenzi, Hospitali ya Rufaa ya KCMC, Polisi, Mahakama na Chama cha Wafanyakazi wa Mashambani (TPAWU).
 
“Watumishi 231 kutoka hospitali ya mkoa ya Mawenzi wamewasilisha malalamiko dhidi ya mwajiri wao kutopeleka michango yake Nssf, Polisi hawajapeleka asilimia 10 kama mchango wake kwa watumishi na idara ya mahakama vivyo hivyo wanachama wake 13 hawaingiziwi michango yao…Lakini pia kuna hospitali ya KCMC, wilaya ya Mwanga na wanachama wa TPAWU wanalia,” alisema Msuya.
 
Akijibu malalamiko hayo, Meneja wa Nssf mkoani Kilimanjaro, Delfina Masika, alisema baadhi ya waajiri hawapo tayari kutoa nafasi kwa shirika hilo kuzungumza na wafanyakazi wao katika maeneo yao jambo ambalo limekuwa likisababishia usumbufu katika kutekeleza majukumu yao.
CHANZO: NIPASHE

0 comments:

 
Supported by Tone Multimedia Company Limited
Copyright © 2012. Kilimanjaro Yetu - All Rights Reserved
Designed by Fredy Tony Njeje
Proudly powered by Blogs za Mikoa