Ikiwa unatukio lolote au jambo lolote tuma kupitia Barua pepe yetu blogzamikoa@live.com au Whatsapp namba +255765056399.
MAHAKAMA ya Hakimu Mkazi Moshi, Kilimanjaro imeelezwa namna
mshitakiwa namba moja katika kesi ya utoroshaji wa wanyama hai 130
wakiwamo twiga wanne kwenda nchi za Falme za Kiarabu, Kamran Ahmed,
raia wa Pakistani alivyopewa idhini ya kufanikisha utoroshaji huo.
Shahidi wa 27 katika kesi hiyo namba 4 ya mwaka 2011, Inspekta
Felichesm Lebule, ambaye ni ofisa upelelezi makosa ya kibinadamu
(Assault Cases), makao makuu ya Polisi Dar es Salaam, aliieleza
mahakama kuwa mshitakiwa alitumia Kampuni ya HAM Marketing ya jijini
Dar es Salaam.
Akitoa ushahidi mbele ya Hakimu Mkazi Mfawidhi, Simon Kobelo, Lebule
alidai kuwa upepelezi uliofanyika mkoani Arusha baada ya kufika ofisi
za Scietest walipata nyaraka za Kampuni ya HAM Marketing inayomilikiwa na mshitakiwa namba mbili, Hawa Mang’unyuka.
Alieleza katika nyaraka hizo ambazo zilikabidhiwa kwao na msimamizi
wa ofisi hiyo, Sylvanus Okudo, walipata maelezo yaliyoonyesha Hawa
alitoa idhini kwa Kamran kwa niaba yake kuendesha shughuli za
usafirishaji pindi awapo nje ya nchi.
“Kilimanjaro na Arusha tulianza kuja tarehe 1 mwezi Machi, 2011,
tulifika pale Scietest Arusha ambapo tulibaini kuwa shughuli zote
zilizokuwa zikifanywa na HAM Marketing zilikuwa zikifanywa na Kamran
kwa niaba ya Hawa,” alieleza Lebule.
Mahakama ilielezwa kuwa baadaye timu ya wapelelezi iliyokuwa
ikiongozwa na Kamishna Msaidizi wa Polisi (ACP), Bunga, ilitoka ofisi
za Scietest na kwenda uwanja wa ndege wa kimataifa Kilimanjaro (KIA),
ambako walifika kwenye Idara ya Forodha na kubaini haikuhusishwa katika
usafirishaji huo.
Akiongozwa na Mwendesha Mashitaka, Wakili wa Serikali, Evetha Mushi,
shahidi huyo aliieleza mahakama kuwa mpango mzima wa usafirishaji wa
wanyama hao haukuhusisha idara hiyo kama sheria zinavyoelekeza na
badala yake ulifanywa na mtu mmoja ambaye ni ofisa mstaafu wa Mamlaka
ya Mapato nchini, aliyemtaja kwa jina la Rajabu Msakamali ambaye
inadaiwa kwa sasa ni marehemu.
“Upelelezi wetu ulibaini kuwa Idara ya Forodha haikuwa na taarifa za
zoezi hili, isipokuwa zoezi zima lilisimamiwa na ofisa mstaafu wa idara
hiyo, Rajabu Msakamali. Msakamali alipostaafu tarehe 30 Juni mwaka
2010, alihama alipokuwa akiishi na kubadilisha namba zote za simu,”
alieleza shahidi na kuongeza:
“Wakati tunamfuatilia huyo Msakamali, nilipokea barua kuhusu kustaafu
kwa mtu huyu, ambayo ilitumwa kwa Mkurugenzi wa Upelelezi Taifa. Barua
hii iliandikwa kutoka makao makuu ya TRA, tarehe 16 mwezi wa tisa
mwaka 2011, yenye kumbukumbu namba TRA/CC/SN/66.”
Kesi hiyo imepangwa kuendelea Agosti 29, mwaka huu kwa upande wa jamhuri kuendelea kuendelea kutoa ushahidi wao.
Inaendelea huku mshitakiwa namba moja, Kamran, akiwa hajulikani aliko
baada ya kushindwa kuhudhuria mahakamani hapo zaidi ya vikao vinne.
Mbali na Kamran Ahmed, washitakiwa wengine ni Hawa Mang’unyuka,
Martin Kimathi na Michael Mrutu, ambao wanadaiwa kusafirisha wanyama
hai Novemba 26, 2010 kwenda Qatar kupitia KIA.
Chanzo;Tanzania Daima
0 comments:
Post a Comment