Home » » WANANCHI MABUNGO WATAKIWA KULIMA MTAMA

WANANCHI MABUNGO WATAKIWA KULIMA MTAMA

Ikiwa unatukio lolote au jambo lolote tuma kupitia Barua pepe yetu blogzamikoa@live.com au Whatsapp namba +255765056399. 
 

WANANCHI wa Kijiji cha Mabungo Wilaya ya Moshi mkoani Kilimanjaro,wametakiwa kulima mazao yanayostahimili hali ya ukame ikiwemo mtama,hatua ambayo itawawezesha kuondokana na tatizo la njaa ambalo limekuwa likiwakumba kila mwaka kutokana na upungufu wa mvua.

Rai hiyo ilitolewa na Mwenyekiti wa Kijiji hicho, Eliahidi Mvanga, wakati akizungumza kwenye mkutano wa kijiji ulioenda sambamba na maadhimisho ya miaka 37 ya kuzaliwa kwa Chama cha Mapinduzi ambapo alisema moja ya mikakati waliyonayo katika kijiji hicho, ni uhamasishaji wa Kilimo cha mtama.

Mvamba alisema kwa zaidi ya miaka mitatu mfululizo sasa, wananchji wa kijiji hicho wamekuwa wakitegemea chakula cha msaada kutokana na mazao yao kukauka kwa kukosa mvua za kutosha, hivyo ni wakati wa wananchi kuondokana na kilimo cha mazoea na kuhakikisha wanalima mtama ili kuweza kukabiliana na tatizo hilo.

"Hali ya ukame imetuathiri kwa kiasi kikubwa wananchi wa Mabungo, na kutokana na hali hii wilaya imetoa agizo wananchi wa maeneo ya ukanda wa chini walime mtama angalau robo heka kila mmoja, na sasa niwatake wananchi, mtekeleze agizo hili na ikiwezekana mlime hata heka moja, ili kuweza kuondokana na tatizo hili la njaa ambalo limekuwa likitusumbua kila mwaka"alisema Mvamba.

Alisema mtama nizao la chakula na biashara, hivyo wananchi wakilima zao hilo wanaweza pia kuondokana na tatizo la umaskini na kufanikiwa kuwapeleka watoto wao shule bila shida wala usumbufu.

"Wananchi wa eneo hili wengi wetu tunategemea kilimo kuyaendesha maisha yetu ya kila siku, sasa mnapaswa kutambua kuwa mtama ni zao la chakula na biashara, na endapo mtaitikia wito huu na kulima zao hili kwa wingi na kwa utaalamu, tutafanikiwa kuwasomesha watoto wetu hadi vyuo vikuu bila usumbufu"alisema.

Mwenyekiti huyo alisema, pamoja na jitihada mbalimbali ambazo wamekuwa wakizifanya katika kuhakikisha wanainua sekta ya kilimo katika kijiji hicho,bado wanakabiliwa na changamoto nyingi ikiwemo upungufu wa pembejeo, hali ambayo imekuwa ikiwafanya wakulima wengi kuendeleza kilimo kisicho na tija.

Alisema Serikali imekuwa ikitoa pembejeo katika kijiji hicho lakini ni chache ikilinganishwa na mahitaji halisi ya wananchi, hivyo kuiomba Serikali kuangalia uwezekano wa kuwaongezea pembejeo, ili kuweza kulima kilimo cha kisasa na ambacho kitawakwamua wananchi kiuchumi.

Wakizungumza baadhi ya wananchi wa kijiji hicho,walisema suala la pembejeo limekuwa ni tatizo kubwa, kutokana na kwamba ambazo zimekuwa zikitolewa na Serikali ni chache sana ambazo hazitoshelezi.

Raihana Shaban aliiomba Serikali kuwaongezea pembejeo za ruzuku,ili kuwawezesha wananchi wote kupata na kuondokana na kilimo cha mazoea.

Chanzo;Majira

0 comments:

 
Supported by Tone Multimedia Company Limited
Copyright © 2012. Kilimanjaro Yetu - All Rights Reserved
Designed by Fredy Tony Njeje
Proudly powered by Blogs za Mikoa